Kimbunga 'Freddy' chaporomosha barabara, kuua watu 100 Malawi

Mji mkuu wa kibiashara wa Malawi wa Blantyre ulirekodi vifo 85. Zaidi ya watu 10,000 waliathiriwa na dhoruba hiyo.

Muhtasari

• Watu wengine 134 walipata majeraha mbalimbali, na 16 wanaripotiwa kupotea baada ya Freddy kuzuka.

• Mji mkuu wa kibiashara wa Malawi wa Blantyre ulirekodi vifo 85

Athari zilizosababishwa na kimbunga Malawi.
Athari zilizosababishwa na kimbunga Malawi.
Image: Getty Images

Wiki jana, taarifa za tahadhari zilisambazwa kote katika mataifa ya Malawi na Madagascar kuhusu uwezekano wa kimbunga Freddy kupiga moja ya mataifa hayo yanayopakana na bahari ya Hindi.

Mapema wiki hii, majarida mbali mbali ya kimataifa yameripoti kuwa kimbunga hicho kilipiga taifa la Malawi na kusababisha hasara kubwa.

AFP waanripoti kwamba takribani watu 100 wamefariki katika athari zilizosababishwa na kimbunga Freddy kilichopiga kata za kusini mwa taifa la Malawi.

“Idadi ya watu waliofariki ikiwamo katika wilaya nyingine zilizokumbwa na maafa katika mikoa ya kanda ya kusini imeongezeka na kufikia 99... lakini tunatarajia idadi hiyo itaongezeka,” Charles Kalemba, kamishna wa Idara ya Masuala ya Kukabiliana na Maafa aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano.

Katika picha zilizosambazwa mitandaoni, barabara zinaonekana zimeporomoka na kuanguka huku mamia ya watu wakiwa wanajikinga kwa miavuli na nguo nzito kutokana na kijibaridi kikali kilichosababishwa na kimbunga Freddy.

Watu wengine 134 walipata majeraha mbalimbali, na 16 wanaripotiwa kupotea baada ya Freddy, ambacho kiko mbioni kuwa moja ya vimbunga vilivyodumu kwa muda mrefu zaidi katika rekodi, kilizuiliwa kusini mwa Afrika mwishoni mwa wiki kwa mara ya pili ndani ya wiki, na kurejea baada ya kupiga mara ya kwanza mwishoni mwa Februari.

Mji mkuu wa kibiashara wa Malawi wa Blantyre ulirekodi vifo 85. Zaidi ya watu 10,000 waliathiriwa na dhoruba hiyo, Kalemba aliambia AFP.

Rais Lazarus Chakwera ametangaza hali ya maafa katika eneo la kusini mwa Malawi.