Malema aongoza maandamano ya kupinga sheria za Uganda dhidi ya mashoga nchini Afrika Kusini

Uganda ilipitisha sheria ya adhabu ya kifo au kifungo cha miaka 20 kwa mashoga.

Muhtasari

•Malema alitangaza kwamba angeongoza maandamano hayo nje ya ofisi za Ubalozi wa Uganda mwendo wa saa tano mchana.

•Malema aliwaalika wafuasi wake kuungana naye katika kupinga sheria hizo zilizopitishwa Uganda wiki chache zilizopita.

Julius Malema
Image: TWITTER// EFF

Leo hii, Aprili 4, kiongozi wa Upinzani wa Afrika Kusini, Julius Sello Malema ameongoza maandamano ya kupinga sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja almaarufu LGBTQ iliyowekwa na serikali ya Uganda.

Siku ya Jumanne asubuhi, Malema ambaye ni kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) alitangaza kwamba angeongoza maandamano hayo nje ya ofisi za Ubalozi wa Uganda mwendo wa saa tano mchana.

"Tuko hapa kutuma ujumbe mkali dhidi ya Mswada wa Kupinga Ushoga nchini Uganda," alisema kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Mwanasiasa huyo mashuhuri aliwaalika wafuasi wake kuungana naye katika kupinga sheria hizo zilizopitishwa Uganda wiki chache zilizopita.

Mwezi uliopita, bunge la Uganda liliidhinisha baadhi ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, ikiwemo adhabu ya kifo na kifungo cha hadi miaka 20 jela kwa watu wanaojitambulisha na LGBTQ+.

Sheria hiyo pia inaweka maisha ya kifungo kwa biashara ya watoto kwa madhumuni ya kuwahusisha watoto katika vitendo vya ushoga.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema kuwa sheria hiyo mpya iliyopitishwa inakwenda kinyume na haki za kimsingi za binadamu na kuitaka serikali kutazama upya utekelezaji wake.

Umoja wa Ulaya (EU) pia ulielezea wasiwasi wake kuhusu Bunge la Uganda kupitisha mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja.

Katika taarifa yake, EU ilisema kuwa inapinga hukumu ya kifo katika hali zote.

Iliongeza kuwa kuharamishwa kwa mahusiano ya jinsia moja ni kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu.

"Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na mamlaka ya Uganda na mashirika ya kiraia ili kuhakikisha kwamba watu wote, bila kujali mwelekeo wao wa kijinsia na utambulisho wa kijinsia, wanahudumiwa kwa usawa, kwa utu na heshima," taarifa hiyo iliendelea kusema.

Wanaharakati wa mashinani na mashirika ya haki za binadamu yamehoji kuwa sheria ina uwezekano wa kuwa na athari zaidi ya watu wanaojitambulisha kuwa wachache wa kingono, na kuathiri maeneo kama vile vyombo vya habari, utoaji wa huduma za afya na haki ya faragha.

Mswada huo hauwi sheria ya uendeshaji hadi Rais Yoweri Museveni atakapoutia saini.