Mbakaji aliyetoroka jela kwa kudanganya kifo akamatwa tena

Thabo alkuwa ameitoroka kwa kuuchoma moto mwili wa mtu mwingine na kuuacha kwenye seli yake.

Muhtasari

•Thabo Bester, anayejulikana kama "mbakaji wa Facebook" alikuwa amejificha kwa karibu mwaka mmoja.

•Thabo Bester alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya mwanamitindo na alitoroka kwa kuuchoma moto mwili wa mtu mwingine na kuuacha kwenye selo yake.

Mwanamume akiwa ametiwa pingu ndani ya seli.
Mwanamume akiwa ametiwa pingu ndani ya seli.
Image: Twitter

Mbakaji aliyepatikana na hatia ambaye alitumia mitandao ya kijamii kuwarubuni waathiriwa wake amekamatwa nchini Tanzania baada ya kutoroka gerezani kwa kudanganya kifo chake.

Thabo Bester, anayejulikana kama "mbakaji wa Facebook" alikuwa amejificha kwa karibu mwaka mmoja.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limethibitisha kukamatwa kwake katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram.

Ni mtu anayesakwa zaidi nchini Afrika Kusini na kutoroka kwake kumelishika taifa hilo. Kumekuwa na taarifa nyingi za kuonekana kwa Thabo Bester katika mwaka uliopita, ikiwa ni pamoja na madai kwamba alionekana akinunua mboga katika kitongoji cha watu matajiri cha Johannesburg.

Lakini wakati huu polisi wa Afrika Kusini wanasema hatimaye wamempata. Katika mkutano na wanahabari, maafisa waliviambia vyombo vya habari Bw Bester alikamatwa siku ya Ijumaa, akiwa na mpenzi wake na mshukiwa wa tatu.

Sasa atarejeshwa Afrika Kusini. Mamlaka ya magereza yamekosolewa vikali, kutokana na kutoroka kwa Bw Bester mnamo Mei mwaka jana. Wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi inayomilikiwa na Uingereza ya G4S, waliokuwa wakiendesha gereza alimokuwa kizuizini, wanatuhumiwa kumsaidia kutoroka.

Thabo Bester alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya mwanamitindo na alitoroka kwa kuuchoma moto mwili wa mtu mwingine na kuuacha kwenye selo yake.

Hapo awali alipatikana na hatia ya kubaka na kuwaibia wanamitindo wawili waliokuwa wamewavutia kwenye mtandao wa Facebook.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu zaidi vya ubakaji duniani, ikiwa na wastani wa matukio 72 kwa kila watu 100,000