Uganda:Mahakama yawanyima dhamana wapenzi wa jinsia moja ili 'kuwalinda'

Wanaume hao wenye umri wa kati ya miaka 20 na 26 walishtakiwa kwa tabia hiyo iliyo kinyume na maadili.

Muhtasari

•Mwendesha mashtaka alisema washukiwa walikuwa sehemu ya mtandao unaowafundisha wavulana wadogo kufanya vitendo vya ulawiti.

•Siku ya Jumanne, Mahakama iliwanyima dhamana kwa misingi kwamba hawatakuwa salama katika jamii.

Image: BBC

Mahakama katika mji wa kusini mwa Uganda wa Jinja umewanyima dhamana wanaume sita wanaotuhumiwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja ambao wanadaiwa kunaswa kwenye video.

Mwendesha mashtaka alisema washukiwa hao walikuwa sehemu ya mtandao unaowafundisha wavulana wadogo kufanya vitendo hivyo vya ulawiti na kuwaingiza wanaume watu wazima katika mahusiano ya mapenzi yajinsia moja, liliripoti gazeti la Daily Monitor.

Wanaume hao wenye umri wa kati ya miaka 20 na 26 walishtakiwa kwa tabia hiyo iliyo kinyume na maadili.

Siku ya Jumanne, Mahakama iliwanyima dhamana kwa misingi kwamba hawatakuwa salama katika jamii.

"Ni jukumu letu kama mahakama kuwalinda washtakiwa. Kuwaachilia huru katika jamii yenye upendeleo hakuwezi kuwahakikishia usalama wao, kwa hivyo gereza ni mahali pao salama,’’ jaji aliamua.

Kesi yao itasikilizwa tarehe 10 Mei.

Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja tayari ni haramu nchini Uganda lakini bunge limependekeza muswada utakaoleta adhabu kali zaidi ikiwemo adhabu ya kifo.