Rais Museveni atia saini muswada dhidi ya wapenzi wa jinsia moja Uganda

Amewataka watekelezaji kutekeleza mamlaka waliyopewa kisheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja.

Muhtasari
  • Aliwashukuru wananchi wa Uganda kwa ''maombi na kutia moyo tulipotekeleza wajibu wetu'' kwa mujibu wa Ibara ya 1 na 79 ya Katiba.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Image: BBC

Spika wa Bunge la Uganda ametangaza kuwa Rais Museveni ameutia saini muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja kuwa sheria.

Spika Anita Among , amesema Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ametekeleza majukumu yake ya kikatiba kama ilivyoainishwa na Ibara ya 91 (3) (a) ya Katiba. Ameidhinisha Sheria ya Kupinga mapenzi ya jinsia moja, aliandika katika taarifa yake aliyoituma kwenye mtandao wa Twitter.

''Kama Bunge la Uganda, tumejibu kilio cha wananchi wetu. Tumetunga sheria ili kulinda utakatifu wa familia kulingana na Kifungu cha 31 cha Katiba ya Uganda''.

''Tumesimama kidete kutetea utamaduni wetu na matarajio ya watu wetu kulingana na malengo ya 19 & 24 ya malengo ya kitaifa na kanuni za maagizo ya sera ya serikali. Namshukuru Mheshimiwa Rais, kwa hatua yake thabiti kwa maslahi ya Uganda.'', aliandika Spika Anita Among.

Aliongeza kuwa ''Kwa Mungu na Nchi yangu, Daima tutasimamia na kuendeleza maslahi ya watu wa Uganda''

Aliwashukuru wananchi wa Uganda kwa ''maombi na kutia moyo tulipotekeleza wajibu wetu'' kwa mujibu wa Ibara ya 1 na 79 ya Katiba.

Amewataka watekelezaji kutekeleza mamlaka waliyopewa kisheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja.

Ikulu ya Uganda katika ukurasa wake wa Twitter imetuma picha ya Museveni kuthibitisha kuwa rais huyo ametia saini muswada:

Uhusiano wa jinsia moja umeharamishwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Lakini mswada wa Kupinga mapenzi ya jinsia moja unalenga kwenda mbali zaidi na kuwafanya watu kuwa wahalifu kwa msingi wa utambulisho wao wa kijinsia.

  • Mtu anayepatikana na hatia ya kulea au kusafirisha watoto kwa madhumuni ya kuwashirikisha katika vitendo vya wapenzi wa jinsia moja anakabiliwa na kifungo cha maisha jela.
  • Watu binafsi au taasisi zinazounga mkono au kufadhili shughuli au mashirika ya haki za LGBT, au kuchapisha, kutangaza na kusambaza nyenzo na fasihi za vyombo vya habari vinavyounga mkono wapenzi wa jinsia moja, pia watakabiliwa na mashtaka na kufungwa gerezani.

Chini ya sheria iliyopendekezwa, marafiki, familia na wanajamii watakuwa na wajibu wa kuripoti watu walio katika mahusiano ya jinsia moja kwa mamlaka.