Zaidi ya watu 280 wafariki, 900 wajeruhiwa katika ajali ya treni nchini India

Treni moja ya abiria inasemekana iliacha njia ya reli kabla ya kugongana na nyingine usiku wa Ijumaa.

Muhtasari

•Zaidi ya magari 200 ya kubebea wagonjwa yalitumwa katika eneo la tukio katika wilaya ya Balasore, anasema katibu mkuu wa Odisha Pradeep Jena.

•Mwanaume mmoja aliyenusurika alisema kwamba "watu 10 hadi 15 waliniangukia wakati ajali ilipotokea na kila kitu kilienda vibaya.

Image: BBC

Takriban watu 288 sasa wamethibitishwa kufarikiwengine 900 kujeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea mashariki mwa jimbo la Odisha nchini India, maafisa wanasema.

Zaidi ya magari 200 ya kubebea wagonjwa yalitumwa katika eneo la tukio katika wilaya ya Balasore, anasema katibu mkuu wa Odisha Pradeep Jena.

Treni moja ya abiria inasemekana iliacha njia ya reli kabla ya kugongana na nyingine usiku wa Ijumaa.

Ni ajali mbaya zaidi ya treni nchini India kuwahi kutokea karne hii. Maafisa wanasema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Shirika la Reli la India lilisema treni mbili zilizohusika katka ajali hiyo ni Coromandel Express na Howrah Superfast Express.

Sudhanshu Sarangi, mkurugenzi mkuu wa Huduma za motp mjini Odisha, alisema kuwa idadi ya waliokufa ilifikia 288.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alisema amesikitishwa na tukio hilo na kutoa pole zake kwa familia zilizofiwa.

"Oparesheni za uokoaji zinaendelea katika eneo la ajali na usaidizi wote unaowezekana unatolewa kwa wale walioathirika," alindika kwenye ukurasa wake wa Tweeter.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani Amit Shah alitaja tukio hilo kuwa la "kuumiza sana".

Mwanaume mmoja aliyenusurika alisema kwamba "watu 10 hadi 15 waliniangukia wakati ajali ilipotokea na kila kitu kilienda vibaya. Nilikuwa chini ya rundo.

"Niliumia mkono na pia nyuma ya shingo yangu. Nilipotoka kwenye bogi ya treni, niliona baadhi ya watu wakiwa wamepoteza mkono, wengine wamepoteza mguu, huku uso wa mtu mwingine ukiwa umeharibika," manusura huyo aliambia shirika la habari la ANI nchini India.

Siku ya maombolezo imetangazwa katika jimbo hilo.