Museveni: Wapenzi wa jinsia moja hawatahukumiwa kwa jinsi walivyo

Ripoti ya wataalamu ilisema kwamba mapenzi ya jinsia moja "ni matokeo ya kuchanganyikiwa kisaikolojia, sio maumbile na sio homoni.

Muhtasari

• Museveni alisema kundi hilo la LGBTQ walio wachache hawatakamatwa ikiwa watatafuta matibabu kwa mfano.

Image: YOWERI MUSEVENI/TWITTER

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa watu wa LGBTQ+ hawatahukumiwa kuwa wahalifu kwa kuwa hivyo tu.

Aliongeza kuwa alipokea ushauri kutoka kwa madaktari wa Uganda na wataalam wengine wa matibabu wakati wa mkutano na Wabunge wa Afrika kutoka nchi 22 za Afrika hivi karibuni, na walihitimisha bila shaka kwamba kuwa mapenzi ya jinsia moja "ni matokeo ya kuchanganyikiwa kisaikolojia, sio maumbile na sio homoni."

Wakati wa hotuba ya kitaifa kwa bunge siku ya Jumatano, Bw. Museveni aliongeza kuwa kundi hilo la walio wachache hawatakamatwa ikiwa watatafuta matibabu kwa mfano.

"Mtu ambaye amechanganyikiwa anaweza kuhitaji usaidizi ili kuondokana na hali ya matatizo ya kiakili," alisema.

Alisisitiza kuwa sheria aliyoitia saini hivi karibuni inaharamisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, kusajili watoto na kupigia upatu mapenzi ya jinsia moja pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.

Rais Museveni pia aliongeza kuwa waajiri au wamiliki wa nyumba hawana haja ya kujua nani anashiriki mapenzi ya jinsia moja au kuwabagua.

Sheria hiyo dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, iliyopitishwa kwa mara ya pili mwanzoni mwa mwezi Mei, imeshutumiwa pakubwa duniani, huku Marekani ikitishia kuiwekea Uganda vikwazo.

Maombi mawili ya kupinga sheria hiyo tayari yamewasilishwa katika mahakama ya kikatiba.

Walalamishi hao wanahoji kuwa ilipitishwa bila ya kuwapa walio wachache nafasi ya kutoa maoni yao na kwamba ni kinyume cha katiba kuharamisha mahusiano ya watu wazima waliokubaliana ya jinsia moja.