Mgogoro wa Sudan: Jinsi watu wanavyozika miili inayoharibika mitaani huko Khartoum

“Nimezika watu watatu ndani ya nyumba yao wenyewe, na wengine katika barabara ya kuingilia ninapoishi," alisema Omar.

Image: GETTY IMAGES

Baada ya wiki kadhaa za mapigano makali ya kudhibiti mji mkuu wa Sudan, baadhi ya wakazi wa Khartoum wanapambana na tatizo wasilolitarajia – wanashughulika na maiti zinazozidi kuongezeka katika mitaa ya jiji.

Onyo: Habari hii ina picha na maelezo ya kukirihisha.

“Nimezika watu watatu ndani ya nyumba yao wenyewe, na wengine katika barabara ya kuingilia ninapoishi," alisema Omar, jina lake tumelibadilisha.

“Kufanya hivyo ni bora, kuliko kufungua mlango na kumuona mbwa anatafuna sehemu ya mwili wa maiti.”

Hakuna anayejua ni watu wangapi wameshafariki hadi sasa, ila inaaminika ni zaidi ya 10000, ikijumuisha wakazi wengi waliojikuta katikati ya mapigano.

Ni hatari kutoka kwenda makaburini. Vikosi viwili vya wanajeshi, Jeshi la kawaida na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), wanapigana licha ya usitishwaji wa mapigano wa mara kadhaa.

Omari ameshazika takribani watu 20. “Jirani yangu aliuawa katika nyumba yake. Sikuweza kufanya chochote zaidi ya kuondoa sakafu ya vigae katika nyumba yake, kuchimba kaburi na kumzika," ameiambia BBC.

“Maiti zinaachwa zioze juani. Nitasema nini? Baadhi ya mitaa ya Khartoum imegeuka kuwa makaburi.”

Mwezi uliopita, Omari alichimba makaburi ya watu wanne pembeni mwa barabara mita chache tu kutoka ilipo nyumba yake katika Wilaya ya Al-Imtidad, Khartoum. Anasema anawajua watu wengine jirani ambao wamefanya hivyo.

“Wengi wa waliofariki walizikwa katika eneo la karibu na chuo kikuu cha Khartoum na kituo cha mafuta, eneo maarufu sana. Maiti nyingine zilizikwa jirani na barabara ya Mohamed Naguib.”

Hakuna takwimu rasmi ya idadi ya watu waliozikwa katika nyumba au mitaa ya Sudan, lakini Omar anasema wanaweza kuwa makumi.

Hamid ambaye jina lake pia limebadilishwa, amepitia hali kama hiyo. Ameiambia BBC, amezika wanajeshi watatu katika eneo la jumuiya la mji wa Shambat, kilomita 12 (maili 7.5), nje ya mji mkuu, baada ya ndege ya kijeshi kuanguka.

“Nilikuwa katika eneo hilo kwa bahati mbaya. Kundi la watu watano nami nikiwemo tulikuwa tunaondoa maiti katika vifusi, na kuwazika katika maeneo yaliyozungukwa na makazi ya watu.”

Hamid, wakala wa mali zisizohamishika ambaye ameishi katika eneo hilo kwa miaka 20, anaamini hii ni kazi ya rehema.

“Muhimu siyo wapi tunawazika wafu. Kuwazika ndio kipaumbele, ni jambo la sadaka ukifanya. Safari ya kwenda makaburini inaweza kuchukua siku, na walenga shabaha wapo kila eneo. Tunajaribu kuisaidia jamii kuepuka janga la magonjwa. Ni wajibu wa kidini na kimaadili.”

Kuuzika Ukweli

Picha hii ya mwili wa mwanajeshi ukiwa umelala barabarani mjini Khartoum inatoka siku ya kwanza ya vita.
Picha hii ya mwili wa mwanajeshi ukiwa umelala barabarani mjini Khartoum inatoka siku ya kwanza ya vita.
Image: REUTERS

Licha ya dhamira njema, bila ya kuja vitendo hivi vinaharibu ushahidi wa uhalifu wa kivita, mkuu wa muungano wa madaktari, Dkt. Attia Abdullah Attia ameeleza.

Ameonya kwamba njia hizi zisizotumia ujuzi, zinaweza kuzika ushahidi. Na kuongeza, na kuharibu kujua namna gani watu walifariki.

Dkt. Attia ameeleza, miili inapaswa kutambuliwa na kuzikwa katika makaburi kwa wakati na njia sahihi. Alisisitiza watu wanapaswa kuliacha suala la mazishi kwa mamlaka za afya, shirika la Msalaba Mwekundu na la Mwezi mwekundu wa Sudan.

“Kuzika miili namna hii hakukubaliki. Katika mchakato wa mazishi, wawakilishi wa serikali wanapaswa kuwepo, wataalamu wa uchunguzi na msalaba mwekundu. Pia, ni muhimu kuchukua sampuli za vinasaba”

Alipoulizwa kwanini anaamini inawezekana kufuata taratibu hizo katika nchi ambayo mfumo wa afya, sheria na taratibu havifanyi tena kazi. Alisema, nchi za nje zinapaswa kuchukua jukumu hilo.

Wazikaji wa kujitolea Omar na Hamid wote wanasema huchukua picha za miili na nyuso zao kabla ya kuwazika, jambo litakalo saidia kuwatambua siku za mbeleni.

Lakini Dkt. Attia anaonya mazishi yasiyo salama yanaweza kuwa chanzo cha kuenea kwa maradhi. “Kuzika katika makaburi yasiyo na kina kirefu, kunatoa uwezekano wa mbwa kufukua maiti. Hapa njia sahihi ya kuzika haifuatwi; kwa sababu kitu kigumu au matofali yanapaswa kuweka juu ya karibu ili kuzuia miili isifichuke.”

Hamid anasema, Wasudani wengi wanajua namna sahihi ya kuchimba kaburi, kwa uchache wa mita moja kwenda chini.

Juhudi rasmi za mazishi

Mwili wa Dk Magdolin Youssef Ghali ulipatikana kando ya dada yake nyumbani kwao Khartoum.
Mwili wa Dk Magdolin Youssef Ghali ulipatikana kando ya dada yake nyumbani kwao Khartoum.
Image: WIZARA YA AFYA YA KHARTOUM/FACEBOOK

Mwanaume tunayemwita Ahmed, anajitolea na Msalaba Mwekundu kuondoa miili katika mitaa.

“Nachukua picha ya nyuso na miili, narekodi ikiwa maiti ni ya muda mfupi na kuipa namba ikiwa maiti imeharibika.” Alisema wanahifadhi faili la kila mwili kwa utambuzi wa baadaye.

Licha ya ukosoaji wa Dkt. Attia, watu huona hawana chaguo kwa sababu ya kuporomoka mfumo wa afya.

Mei 11, video ilisambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha mazishi ya madaktari wawili wa kike wa Sudan katika bustani yao, Magdolin na Madga Youssef Ghali.

Kaka yao ambaye hatutamtaja kwa jina, aliiambia BBC kupitia mazungumzo ya video kwamba, kuwazika dada zake wawili katika nyumba lilikuwa ni suluhisho pekee.

“Waliachwa kwa takribani siku 12 bila ya kuzikwa,” alisema kaka yao akibubujikwa na machozi.

“Majirani waliripoti juu ya harufu kali ikitoka katika nyumba, na ndipo watu walijitolea kuwazika katika kaburi ndani ya bustani.”

Maafisa wa afya wamekuwa wakifanya kazi na shirika la Msalaba Mwekundu na lile la Mwezi Mwekundu, kuondoa miili na kuipeleka makaburini. Lakini mapigano yametatiza kuwasili kwa timu za mazishi.

Wakati watu wakijaribu kujiokoa na kuwazika watu wao kwa njia ya heshima, wazo juu ya mahakama ya uhalifu wa kivita linaonekana kuwa mbali na uwezekano katikati ya vurugu na vifo.

“Dada zangu walizikwa katika kaburi moja katika bustani yao. Sikuwahi kuwaza mwisho wao unaweza kuwa wa namna hiyo,” alisema kaka yao.