Somalia yapiga marufuku TikTok na Telegram

Haya yanajiri huku Somalia ikitangaza lengo kubwa la kuliangamiza kundi la wanamgambo wa al-Shabab

Muhtasari
  • Serikali inasema majukwaa haya yanatumiwa na "magaidi na vikundi vinavyohusika na kueneza uasherati ... kueneza picha za video, picha na kupotosha jamii".
Image: BBC

Somalia imetangaza kupiga marufuku mitandao ya kijamii ya Tiktok na Telegram na jukwaa la kamari la mtandaoni la 1XBet.

Serikali inasema majukwaa haya yanatumiwa na "magaidi na vikundi vinavyohusika na kueneza uasherati ... kueneza picha za video, picha na kupotosha jamii". Haya yanajiri huku Somalia ikitangaza lengo kubwa la kuliangamiza kundi la wanamgambo wa al-Shabab, ambalo bado linadhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo, ndani ya miezi mitano ijayo.

Watoa huduma za mtandao wanatakiwa kutekeleza marufuku hiyo ifikapo Agosti 24 la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria ambazo hazijabainishwa, ilisema taarifa ya wizara ya mawasiliano na teknolojia.

Mkutano wa hivi karibuni wa mtandao na usalama wa mitandao ya kijamii katika mji mkuu, Mogadishu, uliangazia athari mbaya za majukwaa ya mtandaoni kwa vijana, ikiwa ni pamoja na "kusababisha baadhi yao kupoteza maisha".

KWINGINEKO NI KUWA:

Ecowas yapuuzilia mbali mpango wa mpito wa miaka mitatu wa Niger

Jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi, Ecowas, imepuuzilia mbali mbinu ya mazungumzo iliyotangazwa na kiongozi wa mapinduzi ya Niger kwamba utawala wa kiraia hauwezi kurejeshwa kwa miaka mitatu.

Kamishna wa masuala ya kisiasa wa Ecowas, Abdel-Fatau Musa, alisema ratiba hiyo haikubaliki.

Siku ya Jumamosi, Jenerali Abdourahamane Tchiani alisema mazungumzo ya kitaifa yanahitajika ili kuweka misingi ya utaratibu mpya wa kisiasa nchini Niger.

Ecowas imetishia kuchukua hatua za kijeshi kumrejesha madarakani rais aliyeondolewa madarakani.

Umati wa watu umejitokeza tena katika mji mkuu, Niamey, kuunga mkono mapinduzi hayo.

Lakini waandishi wa habari wanasema wengine wanaopinga unyakuzi wa kijeshi wa mamlaka wanaogopa kutoa maoni yao kwa umma.