Mwili wa jambazi Junior Roldán waibwa kutoka makaburini

Alikuwa amekimbilia Colombia baada ya kunusurika majaribio mawili ya kuuawa katika nchi yake ya asili ya Ecuador.

Muhtasari
  • Mabaki ya Junior Roldán yaliwekwa kwenye chumba cha kuhifadhia ukuta katika mji wa Envigado baada ya kutokuwepo na mtu yeyote kudai mwili wake.

Mwili wa kiongozi wa genge la Ecuador umetoweka katika eneo lake la kupumzikia kwenye makaburi huko Colombia, polisi wamesema.

Mabaki ya Junior Roldán yaliwekwa kwenye chumba cha kuhifadhia ukuta katika mji wa Envigado baada ya kutokuwepo na mtu yeyote kudai mwili wake.

Kiongozi huyo wa genge la uhalifu nambari mbili huko Los Choneros, ambalo limekuwa likiitesa Ecuador, alikutwa ameuawa kwa kupigwa risasi katika jimbo la Antioquia nchini Colombia mwezi Mei.

Alikuwa amekimbilia Colombia baada ya kunusurika majaribio mawili ya kuuawa katika nchi yake ya asili ya Ecuador.

Mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha ya risasi kichwani katika eneo la misitu mnamo tarehe 6 Mei.

Polisi wanashuku kuwa aliuawa na mlinzi wake ambaye alitaka kuiba kiasi kikubwa cha fedha alichochukua nacho kiongozi wa genge hilo alipokwenda mafichoni, lakini hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji yake.

Walimtambua kwa tattoo zake na alizikwa kwenye makaburi ya kati kusini mwa Medellín tarehe 18 Mei.

Siku ya Jumanne, wafanyikazi walipata lango la kaburi wazi na walipopekua makaburi hayo waligundua kuwa moja lilikuwa tupu.

Maafisa baadaye walithibitisha kwamba lile lililokuwa wazi lilikuwa na mwili wa Junior Roldán.

Polisi waliviambia vyombo vya habari kuwa watu kadhaa walivamia makaburi hayo usiku na kuuchukua mwili huo.

Kufikia sasa haijabainika iwapo washukiwa hao walikuwa wamelenga mabaki ya kiongozi huyo wa genge hasa na nia yao inaweza kuwa nini.

Roldán alikuwa na maadui wengi.

Kabla ya kutoroka Ecuador, alikuwa amepigwa risasi na kujeruhiwa na washiriki wa genge pinzani linalojiita Los Lobos (The Wolves).