Mwanamfalme Mohammed Bin Salman akariri uungaji mkono wa Saudia kwa Wapalestina

Bin Salman alisema kuwa nchi yake itaendelea "kusimama pamoja na watu wa Palestina ili kufikia haki zao halali za maisha bora.

Muhtasari

•Mtawala mkuu wa Saudi Arabia - Mwanamfalme Mohammed Bin Salman - amezungumza na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kwa simu.

Image: BBC

Mtawala mkuu wa Saudi Arabia - Mwanamfalme Mohammed Bin Salman - amezungumza na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kwa simu.

Bin Salman alisema kuwa nchi yake itaendelea "kusimama pamoja na watu wa Palestina ili kufikia haki zao halali za maisha bora, kufikia matumaini na matarajio yao, na kufikia amani ya haki ya kudumu," Shirika rasmi la Habari la Saudi liliripoti.

Pia alimwambia Abbas kuwa anafanya kazi na pande zote za kimataifa na kikanda kuzuia "kuendelea" kwa mzozo huo.

Inafaa kukumbuka kuwa Abbas na Hamas, ambayo inadhibiti Ukanda wa Gaza, ni wapinzani wa kisiasa.

Abbas anaongoza vuguvugu la Fatah, linalodhibiti Ukingo wa Magharibi. Pia ni mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO).

Lakini uungaji mkono wa Saudi Arabia kwa Wapalestina ni muhimu, kwani inakuja kinyume na msingi wa mazungumzo ya pande tatu yaliyokuwa yakiendelea kati ya Israel, Saudi Arabia na Marekani ili kurejesha uhusiano kati ya Riyadh na Tel Aviv.

Wachambuzi wanasema kuwa mzozo huo unaoongezeka umetoa pigo kubwa kwa mazungumzo ya kuhalalisha.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi baada ya shambulio la Hamas, Saudi Arabia iliishikilia Israel kuhusika na ongezeko hilo.

Ilisema kuwa imetoa "tahadhari za mara kwa mara za hatari ya mlipuko wa hali kutokana na kuendelea kukaliwa kwa mabavu, na kuwanyima watu wa Palestina haki zao halali, na kurudiwa kwa uchochezi wa kimfumo dhidi ya matakatifu yake".