Jamaa auawa na roboti kiwandani ikishindwa kumtofautisha na maboksi ya chakula

Roboti hiyo ilikuwa na jukumu la kuinua masanduku ya pilipili na kuyahamisha kwenye pallets lakini ilishindwa kumtofautisha na boksi na hivyo kumchanganya kwenye mkanda wa kusafirisha mizigo.

Muhtasari

• Jaribio hilo lilikuwa limepangwa kufanyika tarehe 6 Novemba, lakini lilisukumwa mbele kwa siku mbili kutokana na matatizo ya kihisi cha roboti.

• Mwanamume huyo, mfanyakazi kutoka kampuni iliyotengeneza mkono huo wa roboti, alikuwa akiikagua mashine hiyo usiku wa manane siku ya Jumatano ilipoharibika.

Roboti kiwandani
Roboti kiwandani
Image: BBC NEWS

Mwanamume mmoja amebondwa hadi kufa na roboti nchini Korea Kusini baada ya kushindwa kumtofautisha na masanduku ya chakula iliyokuwa ikihudumia, runinga ya BBC News imeripoti Jumatano jioni.

Kisa hicho kilitokea wakati mwanamume huyo, mfanyakazi wa kampuni ya roboti mwenye umri wa miaka 40, alipokuwa akikagua roboti hiyo.

Mkono wa roboti, ukimchanganya mtu huyo kwa sanduku la mboga, ulimshika na kuusukuma mwili wake kwenye mkanda wa kusafirisha mizigo, ukimponda uso na kifua, shirika la habari la Korea Kusini Yonhap lilinukuliwa.

Alipelekwa hospitalini lakini baadaye alifariki.

Kulingana na Yonhap, roboti hiyo ilikuwa na jukumu la kuinua masanduku ya pilipili na kuyahamisha kwenye pallets.

Mwanamume huyo alikuwa akikagua shughuli za sensorer za roboti kabla ya majaribio yake katika kiwanda cha kuchambua pilipili katika mkoa wa Gyeongsang Kusini, uliopangwa kufanyika tarehe 8 Novemba, shirika hilo linaongeza, likiwanukuu polisi.

Jaribio hilo lilikuwa limepangwa kufanyika tarehe 6 Novemba, lakini lilisukumwa mbele kwa siku mbili kutokana na matatizo ya kihisi cha roboti.

Mwanamume huyo, mfanyakazi kutoka kampuni iliyotengeneza mkono huo wa roboti, alikuwa akiikagua mashine hiyo usiku wa manane siku ya Jumatano ilipoharibika.

Katika taarifa baada ya tukio hilo, afisa kutoka Jumba la Kilimo la Donggoseong Export Agricultural Complex, ambalo linamiliki kiwanda hicho, alitaka mfumo "sahihi na salama" uanzishwe.

Mnamo Machi, mwanamume wa Korea Kusini mwenye umri wa miaka 50 alipata majeraha mabaya baada ya kunaswa na roboti alipokuwa akifanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza sehemu za magari.