Waasi wa Colombia wajaribu kuhalalisha utekaji nyara wa baba ya kiungo wa Liverpool, Luis Díaz

Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa (ELN) lilisema lililazimika kumteka nyara ili kupata pesa kwa sababu lilikuwa "maskini".

Muhtasari

•Kiongozi wa waasi wa Colombia, ambao walimshikilia baba yamwanasoka wa Liverpool Luis Díaz, amejaribu kuhalalisha utekaji nyara wake.

•Luis Manuel Díaz na Cilenis Marulanda, walikamatwa kwa mtutu wa bunduki tarehe 28 Oktoba katika mji alikozaliwa wa Barrancas.

Image: BBC

Raia wa Colombia wamejawa na hasira baada ya kiongozi wa waasi wa Colombia, ambao walimshikilia babake mwanasoka wa Liverpool Luis Díaz, kujaribu kuhalalisha utekaji nyara wake.

Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa (ELN) lilisema lililazimika kumteka nyara ili kupata pesa kwa sababu lilikuwa "maskini".

Kundi hilo limekuwa likifanya mazungumzo ya amani kwa karibu mwaka mmoja.Kutekwa nyara kwa babake Luis Díaz, kocha mahiri wa mpira wa miguu, kumezua shaka juu ya kujitolea kwake kwa mazungumzo.

Wazazi wa mwanasoka huyo, Luis Manuel Díaz na Cilenis Marulanda, walikamatwa kwa mtutu wa bunduki tarehe 28 Oktoba katika mji alikozaliwa wa Barrancas, kaskazini mwa jimbo la La Guajira.

Watekaji nyara walimwachilia Bi Marulanda ndani ya gari saa chache baadaye huku vikosi vya usalama vya Colombia, wanajeshi na polisi, wakiwakaribia watekaji nyara.

Lakini waasi hao walimshikilia Luis Manuel Díaz mwenye umri wa miaka 58 kwa siku 12 kabla ya kumwachilia kwa ujumbe unaojumuisha maafisa kutoka Umoja wa Mataifa na Kanisa Katoliki.

Kamanda wa waasi wa ELN Antonio García amesimama kidete kwenye msimamo wa ELN kuhusu utekaji nyara tangu Luis Manuel Díaz aachiliwe.

Kamanda wa waasi alisisitiza kuwa utekaji nyara kwa ajili ya fidia sio ukiukaji wa usitishaji mapigano ambao kundi lake lilikuwa limetia saini, ambao ulianza kutumika mnamo Agosti.

Bwana García hapo awali alidai kwamba kulengwa kwa babake mwanasoka huyo maarufu lilikuwa "kosa".

"Hakuna makubaliano yoyote ambayo ELN imejitolea kujizuia na shughuli za kifedha, ikiwa ni pamoja na kumnyima mtu uhuru wake kwa sababu za kiuchumi," aliandika katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.