Sierra Leone chini ya amri ya kutotoka nje baada ya wafungwa kutoroshwa

Wafungwa wametoroshwa kutoka gereza moja nchini Sierra Leone kufuatia milio ya risasi katika mji mkuu Freetown

Muhtasari

•Amri ya kutotoka nje nchini kote imetangazwa baada ya watu wenye silaha kujaribu kuingia kwenye hifadhi ya silaha ya kambi moja ya kijeshi iliyo karibu na makao makuu ya rais.

Image: BBC

Wafungwa wametoroshwa kutoka gereza moja nchini Sierra Leone huku kufuatia milio ya risasi katika mji mkuu Freetown asubuhi ya leo. Amri ya kutotoka nje nchini kote imetangazwa baada ya watu wenye silaha kujaribu kuingia kwenye hifadhi ya silaha ya kambo moja ya kijeshi iliyo karibu na makao makuu ya rais.

Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, alithibitisha ripoti za walioshuhudia kwamba watu hao wenye silaha walivamia gereza la Central Pademba Road mjini Freetown na kuwaachilia baadhi ya wafungwa.

Haijabainika ni wafungwa wangapi walifanikiwa kutoroka. Habari hizo zinakuja baada ya mamlaka kutaka kuwatuliza raia, na kusema kuwa hali imedhibitiwa. Katika taarifa iliyoripotiwa kuandikwa kutoka nyumbani kwake asubuhi ya leo, Rais Julius Maada Bio alisema kuwa utulivu umerejeshwa na msako umeanzishwa ili kuwakamata wahusika wengine. Lakini mwandishi wa BBC mjini Freetown anasema hali bado inaonekana kuwa tete.

Aliwapita askari waliokuwa wamebeba silaha nzito katika gari la polisi lililokamatwa, na kuona wengine wakiimba kwamba wanapanga "kusafisha Sierra Leone". Marekani na Jumuiya ya kikanda ya ECOWAS wamelaani ghasia hizo.

Mwezi Juni rais Julius Maada Bio alichaguliwa tena baada ya kuepuka duru ya pili ya uchaguzi. Mwezi Agosti, watu kadhaa, wakiwemo askari wa vyeo vya juu walikamatwa na kutuhumiwa kupanga mapinduzi dhidi ya rais. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita nchi kadhaa za Afrika Magharibi na kati zimefanya mapinduzi, ikiwa ni pamoja na nchi jirani ya Guinea ambayo kwa sasa iko chini ya utawala wa kijeshi