Glynn Simmons: Mtu aliyefungwa jela kwa muda mrefu zaidi Marekani afutiwa hatia miaka 48 baadaye

Glynn Simmons, 70, aliachiliwa huru mwezi Julai wakati hakimu alipoamuru kesi mpya isikilizwe.

Muhtasari

•Jaji wa Oklahoma amemuondolea mashtaka mtu ambaye alikuwa gerezani kwa karibu nusu karne kwa mauaji ya 1974.

•Bw Simmons alikuwa na umri wa miaka 22 wakati yeye na mshtakiwa mwenzake, Don Roberts, walipopatikana na hatia.

Image: BBC

Jaji wa Oklahoma amemuondolea mashtaka mtu ambaye alikuwa gerezani kwa karibu nusu karne kwa mauaji ya 1974, kifungo kirefu zaidi cha makosa kutumikiwa Marekani.

Glynn Simmons, 70, aliachiliwa huru mwezi Julai wakati hakimu alipoamuru kesi mpya isikilizwe.

Lakini wakili wa wilaya alisema siku ya Jumatatu hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kutoa idhini.

Katika agizo mnamo Jumanne, Jaji wa Wilaya ya Oklahoma County Amy Palumbo alimtangaza Bw Simmons kuwa hana hatia.

"Mahakama hii inapata kwa ushahidi wa wazi na wa kuridhisha kwamba kosa ambalo Bw Simmons alitiwa hatiani, alihukumiwa na kufungwa... halikufanywa na Bw Simmons," alisema katika uamuzi wake.

"Ni somo katika uthabiti na ukakamavu," Bw Simmons aliwaambia wanahabari baada ya uamuzi huo, kulingana na Associated Press. "Usiruhusu mtu yeyote akuambie kwamba haiwezi kutokea, kwa sababu inaweza kweli."

Bw Simmons alikuwa ametumikia kifungo cha miaka 48, mwezi mmoja na siku 18 gerezani kwa mauaji ya Carolyn Sue Rogers wakati wa wizi wa duka la pombe katika kitongoji kimoja na jiji la Oklahoma . Hilo linamfanya kuwa mfungwa aliyetumikia kifungo kwa muda mrefu zaidi kuachiliwa, kulingana na Msajili wa Kitaifa wa Waliosamehewa.

Bw Simmons alikuwa na umri wa miaka 22 wakati yeye na mshtakiwa mwenzake, Don Roberts, walipopatikana na hatia na kuhukumiwa kifo mwaka wa 1975.

Adhabu hizo baadaye zilipunguzwa hadi kifungo cha maisha jela kwa sababu ya maamuzi ya Mahakama ya Juu ya Marekani kuhusu hukumu ya kifo.

Bwana Simmons alikuwa amesema alikuwa katika jimbo lake la Louisiana wakati wa mauaji hayo.

Mahakama ya wilaya ilifuta kifungo chake mwezi Julai baada ya kupata kwamba waendesha mashitaka hawakukabidhi ushahidi wote kwa mawakili wa upande wa utetezi, ikiwa ni pamoja na kwamba shahidi alikuwa amewatambua washukiwa wengine.

Bw Simmons na Bw Roberts walihukumiwa kwa sehemu kwa sababu ya ushuhuda kutoka kwa kijana ambaye alikuwa amepigwa risasi nyuma ya kichwa. Kijana huyo aliwanyooshea kidole wanaume wengine kadhaa wakati wa safu za polisi za kuwatambua washukiwa .

Bw Roberts aliachiliwa kwa msamaha mwaka wa 2008.

Watu waliohukumiwa kimakosa wanaohudumu huko Oklahoma wanastahiki hadi $175,000 (£138,000) kama fidia.

Bw Simmons kwa sasa anapambana na saratani ya ini, kulingana na GoFundMe yake, ambayo imechangisha maelfu ya dola kusaidia gharama zake za maisha na matibabu ya saratani.