Kampuni ya meli ya Maersk inajiandaa kurejelea shughuli zake katika Bahari Nyekundu

Njia mbadala, karibu na Rasi ya Good Hope, inaongeza takriban maili 3,500 za baharini kwa safari.

Muhtasari
  • Hatua hiyo inafuatia kuanzishwa kwa operesheni ya kijeshi ya kimataifa kuzuia mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara na waasi wa Houthi wa Yemen.
Image: REUTERS

Kampuni kubwa ya meli ya Denmark ya Maersk imesema inajiandaa kurejesha shughuli za meli kupitia Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden.

Hatua hiyo inafuatia kuanzishwa kwa operesheni ya kijeshi ya kimataifa kuzuia mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara na waasi wa Houthi wa Yemen.

Makampuni kadhaa yamesitisha usafirishaji bidhaa kupitia Bahari Nyekundu kufuatia mashambulio hayo.

Kampuni ya usafirishaji ya Ujerumani ya Hapag-Lloyd imesema itaamua Jumatano ikiwa itaanza tena kutumia njia hiyo.

Bahari Nyekundu ni mojawapo ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa, na pia kwa bidhaa za watumiaji.

Imehifadhiwa na Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab - unaojulikana pia kama Lango la Machozi - kusini karibu na pwani ya Yemen na Mfereji wa Suez kaskazini.

Wahouthi wametangaza kuunga mkono Hamas katika vita vyake na Waisraeli, na waasi walioko Yemen wamesema wanalenga meli ambazo wanaamini zinaelekea Israel.

Baadhi ya meli zimeshambuliwa na ndege zisizo na rubani na roketi.

Njia mbadala, karibu na Rasi ya Good Hope, inaongeza takriban maili 3,500 za baharini kwa safari.

Hii imesababisha hofu ya kukatizwa kwa usambazaji wa bidhaa zinazosafirishwa kupitia Mfereji wa Suez, na kuongezeka kwa bei ili kufidia gharama kubwa za usafirishaji.