Serikali ya DRC yapiga marufuku maandamano ya upinzani yanayotarajiwa leo

Wagombea kadhaa wa upinzani wameitisha maandamano ya umma leo Jumatano

Muhtasari
  • Miongoni mwa viongozi hao wa upinzani Martin Fayulu amesema wataandamana katika mji mkuu Kinshasa kupinga uchaguzi alioutaja uliojaa udanganyifu.
Image: REUTERS

Wakati upinzani nchini DRC ukitangaza msururu wa maandamano kuanzia hii leo , serikali kupitia Naibu waziri mkuu nchini humo Peter Kazadi amesema kuwa serikali haitakubali maandaano hayo kufanyika.

Bw. Kazadi ambaye pia anasimamia wizara ya mambo ya ndani nchini DRC ameuambia upinzani nchini humo kwamba yeyote mwenye pingamizi kuhusu matokeo anastahili kuwasilisha malalamiko mahakamani na kwamba Serikali haitavumilia uharibifu wowote .

Kwa sasa matokeo ya Kiti cha Urais yanaonesha Rais Felix Tshisekedi bado anaongoza kwa kura .

Wagombea kadhaa wa upinzani wameitisha maandamano ya umma leo Jumatano kupinga jinsi tume ya uchaguzi CENI ilivyoendesha uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 20 mwezi huu.

Miongoni mwa viongozi hao wa upinzani Martin Fayulu amesema wataandamana katika mji mkuu Kinshasa kupinga uchaguzi alioutaja uliojaa udanganyifu.

Usalama umeimarishwa katika maeneo mengi ya DRC. Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais yaliyotangazwa na CENI yanaonesha Rais Felix Tshisekedi anayetafuta muhula wa pili madarakani akiongoza.