Waziri wa zamani wa Zanzibar ahojiwa kuhusu uhaba wa pombe kisiwani humo

Alikuwa amejiuzulu kama waziri wa utalii wiki mbili zilizopita, akitaja "mazingira yasiyopendeza na ya kutatiza ya kazi".

Muhtasari

•Simai Mohamed Said alifika mbele ya kamati ya maadili ya chama hicho siku ya Jumanne lakini hakufichua kwanini aliitwa.

Image: BBC

Chama tawala cha Tanzania (CCM) kimemuhoji aliyekuwa waziri wa utalii wa Zanzibar wiki kadhaa baada ya kujiuzulu kutokana na uhaba wa pombe visiwani humo.

Simai Mohamed Said alifika mbele ya kamati ya maadili ya chama hicho siku ya Jumanne lakini hakufichua kwanini aliitwa.

"Ni kawaida kutembelea afisi ya chama, na mimi si msemaji wa mikutano, unaweza kupata mwenyekiti au katibu mkuu wa kamati kusema jambo," Bw Said aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo.

Alikuwa amejiuzulu kama waziri wa utalii wiki mbili zilizopita, akitaja "mazingira yasiyopendeza na ya kutatiza ya kazi".

Kujiuzulu kwake kumehusishwa na uhaba wa pombe unaovikabili visiwa hivyo vya Tanzania, jambo ambalo linatishia sekta ya utalii ya mojawapo ya maeneo yanayoongoza kwa utalii barani Afrika.

Bei za bia zimepanda kwa karibu 100% baada ya msururu wa usambazaji kutatizwa na mabadiliko ya ghafla ya waagizaji.

Kabla ya kujiuzulu, Bw Said aliituhumu hadharani Bodi ya Kudhibiti Vileo Zanzibar (ZLCB) kwa kusimamia vibaya idara ya vileo.

Lakini Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi alimshutumu Bw Said kwa kuwa na mgongano wa kimaslahi, alipokuwa waziri.

Ripoti zinahusisha jamaa mmoja wa Bw Said na kampuni moja ya kuagiza pombe ambayo leseni yake haikuongezwa ili kuendelea kuhudumu.

Upungufu huo wa pombe unakuja huku kukiwa na ongezeko la watalii wanaowasili katika visiwa vya Tanzania.