Makumi ya watu wajeruhiwa katika mlipuko magharibi mwa Cameroon

Tukio hilo lilitokea Jumapili wakati wanafunzi hao wakiandamana kuadhimisha siku ya vijana nchini.

Muhtasari

•Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha wanafunzi wakikimbilia usalama baada ya mlipuko huo.

Image: BBC

Mwanafunzi mmoja amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya bomu kulipuka katika eneo la Kaskazini-Magharibi la Cameroon.

Tukio hilo lilitokea Jumapili wakati wanafunzi hao wakiandamana kuadhimisha siku ya vijana nchini katika mji wa Nkambe.

Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha wanafunzi wakikimbilia usalama baada ya mlipuko huo.

Mkuu wa mkoa aliviambia vyombo vya habari vya serikali kuwa mwanafunzi mmoja aliuawa na watu 40 walijeruhiwa katika tukio hilo.

Gavana Adolphe Lele L'Afrique alisema wapiganaji wanaotaka kujitenga wanashukiwa kufanya shambulio hilo.

Wapiganaji hao wa Anglophone walikuwa wameweka kizuizi ili kutatiza sherehe hizo.

Mashambulizi dhidi ya wanafunzi, walimu na taasisi za elimu ni ya kawaida katika eneo la Cameroon ambalo wakazi wake wanazungumza lugha ya Kiingereza.

Tukio hilo linaonekana kama jaribio la wapiganaji hao kutekeleza mgomo wao dhidi ya elimu, ambayo waliiweka zaidi ya miaka saba iliyopita.

Kwanini Cameroon bado imegawanyika kwa misingi ya ukoloni?

  • Ilitawaliwa na Ujerumani mwaka 1884
  • Majeshi ya Uingereza na Ufaransa yaliwalazimisha Wajerumani kuondoka mwaka 1916
  • Cameroon iligawanyika mara tatu miaka iliyofuatia- 80% ikaenda kwa Ufaransa na 20% ikaenda Uingereza
  • Cameroon iliyoyoendeshwa na Ufaransa ikawa huru mwaka 1960
  • Kufuatia kura ya maoni , eneo la Uingereza Kusini likajiunga na Cameroon na WaCameroon wa Kaskazini wakajiunga na Nigeria inayozungumza kiingereza.