Ufaransa yafanya uavyaji mimba kuwa haki ya kikatiba

Imekuwa nchi ya kwanza duniani kujumuisha kwa uwazi haki ya utoaji mimba katika katiba yake.

Muhtasari

•Wabunge walipiga kura kurekebisha katiba ya nchi ya 1958 ili kuweka "uhuru uliohakikishwa" wa wanawake wa kutoa mimba.

Image: BBC

Ufaransa imekuwa nchi ya kwanza duniani kujumuisha kwa uwazi haki ya utoaji mimba katika katiba yake.

Wabunge walipiga kura kurekebisha katiba ya nchi ya 1958 ili kuweka "uhuru uliohakikishwa" wa wanawake wa kutoa mimba.

Kura nyingi za 780-72 zilishuhudia shangwe kubwa katika bunge la Versailles wakati matokeo yalipotangazwa.

Rais Emmanuel Macron alielezea hatua hiyo kama "fahari ya Ufaransa" ambayo ilituma "ujumbe wa ulimwengu wote".

Hata hivyo makundi yanayopinga uavyaji mimba yamekosoa vikali mabadiliko hayo, kama ilivyofanya Vatican.

Uavyaji mimba umekuwa halali nchini Ufaransa tangu 1975, lakini kura za maoni zinaonesha karibu 85% ya umma waliunga mkono marekebisho ya katiba ili kulinda haki ya kumaliza ujauzito.

Na wakati nchi nyingine kadhaa zinajumuisha haki za uzazi katika katiba zao, Ufaransa ndiyo ya kwanza kusema kwa uwazi kwamba utoaji mimba utahakikishwa.

Kufuatia kura hiyo, Mnara wa Eiffel mjini Paris uliangaziwa katika sherehe, ukiwa na ujumbe: "My Body My Choice".

Kabla ya kura hiyo, Waziri Mkuu Gabriel Attal aliliambia bunge kwamba haki ya kutoa mimba inasalia "katika hatari" na "kwa huruma ya watoa maamuzi".

"Tunatuma ujumbe kwa wanawake wote: mwili wako ni wako na hakuna anayeweza kukuamulia," aliongeza.