Marekani yawahamisha wafanyakazi wa ubalozi Haiti huku kukiwa na vurugu za magenge

Wamarekani pia wameimarisha usalama katika misheni yao katika mji mkuu, Port-au-Prince.

Muhtasari

•Hatua hii inafuatia mashambulizi ya magenge kwenye uwanja wa ndege, vituo vya polisi na magereza wiki jana.

•Bandari kuu nchini humo ilisema kuwa inasitisha shughuli zake siku ya Alhamisi kutokana na hujuma na uharibifu.

Image: BBC

Marekani inasema imewasafirisha kwa ndege wafanyakazi wasio wa lazima wa ubalozi kutoka Haiti, huku nchi hiyo ikizidi kutumbukia katika ghasia za magenge.

Wamarekani pia wameimarisha usalama katika misheni yao katika mji mkuu, Port-au-Prince.

Hatua hii inafuatia mashambulizi ya magenge kwenye uwanja wa ndege, vituo vya polisi na magereza wiki jana. Wanashinikiza kuondolewa kwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry.

Hali ya hatari ya siku tatu imeongezwa kwa mwezi.

"Kuongezeka kwa ghasia za magenge katika kitongoji karibu na majengo ya ubalozi wa Marekani na karibu na uwanja wa ndege kulisababisha uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Nje kupanga kuondoka kwa wafanyakazi wa ziada wa ubalozi," ubalozi huo uliweka taarifa hiyo kwenye mtandao wa kijamii.

Iliongeza kuwa ubalozi huo utabaki wazi.

Operesheni hiyo ilionekana kuendeshwa na helikopta, shirika la habari la AFP linaripoti, likiwanukuu wakaazi wa karibu ambao walielezea kusikia sauti za ndege ikiapaa juu ya makazi yao.

Siku ya Jumapili, balozi wa Ujerumani nchini Haiti pia aliondoka, akisafiri kuelekea Jamhuri ya Dominika, pamoja na wawakilishi wengine wa Umoja wa Ulaya, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani iliambia AFP.

Hatua hii inawadia huku hali nchini Haiti ikizidi kuwa mbaya.

Bandari kuu nchini humo ilisema kuwa inasitisha shughuli zake siku ya Alhamisi kutokana na hujuma na uharibifu.

Magenge katika jiji hilo lililokumbwa na ghasia yalizidisha mashambulizi yao wakati Bw Henry alipoondoka kwa mkutano wa kilele wa kanda wiki jana.

Bwana Henry alijaribu kurudi Port-au-Prince siku ya Jumanne lakini akaishia katika eneo la Marekani la Puerto Rico badala yake.

Hakuweza kutua katika mji mkuu wa Haiti kwa sababu uwanja wake wa ndege wa kimataifa ulifungwa huku wanajeshi wakizuia majaribio ya watu wenye silaha kutaka kuuteka.

Mamlaka ya usafiri wa anga katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominika pia iliikataa ndege ya waziri mkuu huyo kutua, ikisema kwamba hawakupewa mpango unaohitajika wa safari.

Bw Henry hajatoa taarifa zozote kwa umma tangu alipozuru Kenya, ambapo alikutana na Rais William Ruto ili kuokoa makubaliano ya nchi hiyo ya Afrika mashariki kuongoza jeshi la mataifa mbalimbali kusaidia kurejesha utulivu nchini Haiti.