Maelfu ya wanandoa wapya Zimbabwe wagundua vyeti vyao vya ndoa ni batili

Wanandoa wengi waliooana hivi karibuni nchini Zimbabwe wameshangaa kujua kwamba vyeti vyao vya ndoa si halali.

Muhtasari

•Imeibuka kuwa, kwa sababu ya suala la ukarani, vyeti vilivyotolewa ndani ya miezi 18 iliyopita ni batili.

•Wanasheria pia walionya ikiwa una cheti batili huwezi kupata talaka.

Image: BBC

Maelfu ya waliooana hivi karibuni nchini Zimbabwe wameshangaa kujua kwamba vyeti vyao vya ndoa si halali.

Imeibuka kuwa, kwa sababu ya suala la ukarani, vyeti vilivyotolewa ndani ya miezi 18 iliyopita ni batili, ugunduzi ambao unaweza kuathiri wanandoa wote waliofunga ndoa ndani ya kipindi hiki.

Jambo hilo lilikuja kujulikana wakati Chama cha Wanasheria cha Zimbabwe kilitoa notisi ya tahadhari kwa wanasheria kote nchini.

Kilibainisha kuwa vifaa vya kuandikia vinavyotumika kwenye vyeti vya ndoa vya kiraia vinaendelea kunukuu sura ya sheria ya zamani ya ndoa ambayo ilibatilishwa mnamo mwaka 2022.

Sheria mpya, ambayo ilianza kutumika Septemba 2022, ilileta mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na haki kwa wapenzi katika ndoa za kitamaduni. Pia iliharamisha ndoa za utotoni.

Chama cha wanasheria kimewashauri walioathirika kupeleka vyeti vyao kwa msajili ambaye atarekebisha na kugonga muhuri wa hati hiyo.

Wanasheria pia walionya ikiwa una cheti batili huwezi kupata talaka.

Wapenzi kadhaa waliooana hivi karibuni ambao walizungumza na BBC hawakujua hapo awali kwamba vyeti vyao vinaweza kuwa batili.

Mkanganyiko huo uliibua gumzo kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii, huku wengine wakitania ilikuwa fursa kwa wale wanaotafuta njia ya kutoka nje ya ndoa zao.

Idara ya Usajili wa Kiraia iliambia jarida linalomilikiwa na serikali The Chronicle kwamba ingawa inaweza kurekebisha vyeti vilivyopo, haiwezi kuchapisha maandishi mapya yenye sheria sahihi bila serikali kwanza kutangaza mabadiliko hayo kupitia gazeti la serikali.