Uchaguzi Senegal: Kiongozi wa upinzani Faye yuko kifua mbele kushinda urais

Mamilioni ya watu walishiriki katika upigaji kura wa amani siku ya Jumapili.

Muhtasari

•Diomaye Faye ameibuka kuwa anayepewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa urais nchini Senegal, baada ya wapinzani kadhaa kukubali kushindwa.

•Bw Faye, 44, mwanachama wa chama cha Pastef kinachoongozwa na Ousmane Sonko, alikuwa gerezani siku chache kabla ya uchaguzi.

Image: BBC

Kiongozi wa upinzani Bassirou Diomaye Faye ameibuka kuwa anayepewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa urais nchini Senegal, baada ya wapinzani kadhaa kukubali kushindwa.

Mamilioni ya watu walishiriki katika upigaji kura wa amani siku ya Jumapili, kufuatia miaka mitatu ya misukosuko na maandamano ya upinzani dhidi ya aliyemaliza muda wake, Macky Sall.

Wapiga kura walikuwa na chaguo la wagombea 19.

Hata hivyo, chaguo la muungano unaotawala, Amadou Ba, alikanusha ripoti za kushindwa na kusema kuwa anatazamia kushiriki katika duru ya pili ya kura ili kuamua mshindi.

Bw Faye, 44, mwanachama wa chama cha Pastef kinachoongozwa na Ousmane Sonko, alikuwa gerezani siku chache kabla ya uchaguzi. Bw Sonko aliondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa sababu ya kukutwa na hatia ya kumharibia jina.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa kwenye televisheni yalionyesha Bw Faye amepata kura nyingi, na hivyo kusababisha sherehe kubwa mitaani katika mji mkuu wa Dakar.

Wafuasi walianza kurusha fataki, kupeperusha bendera za Senegal na kupuliza mavuvuzela.

Matokeo hayo pia yalipelekea wagombea watano wa upinzani kumtangaza Bw Faye kuwa mshindi. Anta Babacar Ngom, mmoja wa waliotangulia, alimtakia mafanikio Bw Faye katika taarifa yake.

Bw Sonko alimuunga mkono Bw Faye, mwanzilishi mwenza wa chama chake kilichofutwa cha Pastef, ambaye pia alizuiliwa takriban mwaka mmoja uliopita kwa mashtaka yakiwemo ya kukashifu na kudharau mahakama.

Sheria ya msamaha iliyopitishwa mwezi huu iliruhusu kuachiliwa kwao kabla ya siku ya kupiga kura.

Wamefanya kampeni pamoja chini ya bango "Diomaye ni Sonko". Baadhi ya wanasiasa mashuhuri na wagombeaji wa upinzani wameunga mkono kugombea kwa Bw Faye.