Waziri mpya wa nishati Uganda adai alitabiriwa kuhusu uteuzi wake miaka 3 iliyopita na mchungaji

Wakati huo, alisema, alikuwa ametoka tu kushinda kiti cha ubunge, wakati mchungaji alipomwekea mikono na kutabiri uteuzi wake kwenye baraza la mawaziri.

Muhtasari

• Katika ibada hiyo, Nyamutoro alifichua kwamba alifahamu kuhusu uteuzi wake kupitia rafiki yake aliyeko USA.

Phiona Nyamutoro
Phiona Nyamutoro
Image: Screengrab//YT

Waziri mpya wa nishati nchini Uganda, Phiona Nyamutoro amezua gumzo katika mitandao ya kijamii nchini humo baada ya kusimama kidete na kudai kwamba uteuzi wake serikalini kama waziri ulitabiriwa na mchungaji miaka 3 iliyopita.

Nyamutoro aliteuliwa na rais Yoweri Museveni kama waziri mpya wa Nishati na Madini alifichua hayo Jumapili wakati anazungumza kwenye ibada kanisani.

Nyamutoro, ambaye pia ni mbunge wa vijana kitaifa bungeni, alifichua jana kuwa uteuzi wake ulitabiriwa takriban miaka mitatu iliyopita na Mchungaji kwa jina Robert Kayanja wa Rubaga Miracle Centre.

Wakati huo, alisema, alikuwa ametoka tu kushinda kiti cha ubunge, wakati mchungaji alipomwekea mikono na kutabiri uteuzi wake kwenye baraza la mawaziri.

"Nakumbuka nilipokuja kutoa shukrani nilipokuwa nimepigiwa kura kuwa mbunge wa kitaifa, Mchungaji, uliniwekea mikono na kutangaza kwamba nitateuliwa kuwa waziri," alisema.

“Sasa niko hapa kutoa ushahidi kwamba Alhamisi niliteuliwa kuwa waziri wa Nishati (mwenye dhamana ya madini). Ninataka kusema kwamba kuna Mungu mbinguni ambaye anaendesha mambo ya wanadamu na kwamba Mungu ndiye Mungu wa Kituo cha Miujiza,” alisema huku kanisani likipiga makofi.

Katika ibada hiyo, Nyamutoro alifichua kwamba alifahamu kuhusu uteuzi wake kupitia rafiki yake aliyeko USA.

Aliahidi kurudi kanisani kutoa Shukrani ifaayo baada ya kuapishwa.