Serikali ya Israel yasema itaizuia Al Jazeera kutangaza nchini humo

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema "atachukua hatua mara moja" ili kufunga ofisi ya ndani ya shirika hilo.

Muhtasari

•Bunge la Israel limeidhinisha sheria inayoipa serikali mamlaka ya kupiga marufuku matangazo ya chaneli za TV ikiwemo Al Jazeera.

Mtoto wa mkuu wa ofisi ya Al Jazeera Gaza Wael Al-Dahdouh (pichani) aliuawa katika shambulio la Israeli mnamo Januari.
Mtoto wa mkuu wa ofisi ya Al Jazeera Gaza Wael Al-Dahdouh (pichani) aliuawa katika shambulio la Israeli mnamo Januari.
Image: BBC

Bunge la Israel limeidhinisha sheria inayoipa serikali mamlaka ya kupiga marufuku matangazo ya chaneli za TV ikiwemo Al Jazeera, mtandao unaomilikiwa na taifa la Qatar.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema "atachukua hatua mara moja" ili kufunga ofisi ya ndani ya mtandao huo.

Marekani ilionyesha wasiwasi wake kuhusu hatua hiyo.Huku waandishi wa habari wa kigeni wakipigwa marufuku kuingia Gaza, wafanyakazi wa Al Jazeera walioko kwenye ukanda huo wamekuwa baadhi ya waandishi pekee walioweza kuandika habari za vita hivyo mashinani.

Bunge la Knesset, Bunge la Israel, liliidhinisha mswada huo unaoruhusu mitandao ya kigeni inayozingatiwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa kupigwa marufuku "kwa muda".Marufuku hiyo ingewekwa kwa muda wa siku 45 kwa wakati mmoja, ambayo inaweza kuongezwa upya.

Sheria hiyo itaendelea kutumika hadi Julai au hadi mwisho wa mapigano makubwa huko Gaza."

Al Jazeera haitatangaza tena kutoka Israel," Bw Netanyahu aliandika kwenye Twitter/X, akiuita mtandao huo "chaneli ya kigaidi".Kwa miaka mingi, maafisa wa Israel wamekuwa wakishutumu mtandao huo kwa chuki dhidi ya Israel.

Lakini ukosoaji wao kwa shirika hilo la utangazaji umeongezeka tangu mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba.

Mamlaka zinadai kuwa ina uhusiano wa karibu na Hamas, ambayo Al Jazeera inakanusha vikali.

Katika taarifa, Al Jazeera ilisema: "Netanyahu hakuweza kutoa sababu za haki kwa ulimwengu kwa mashambulizi yake yanayoendelea dhidi ya Al Jazeera na uhuru wa vyombo vya habari isipokuwa kuwasilisha uongo mpya na kashfa za uchochezi dhidi ya Mtandao na haki za wafanyakazi wake.

"Al Jazeera inamshikilia Waziri Mkuu wa Israeli kuwajibika kwa usalama wa wafanyikazi wake na majengo ya Mtandao huo kote duniani, kufuatia uchochezi wake na tuhuma hii ya uwongo kwa njia ya aibu."