Marekani yaiambia Israel kuwa haitashiriki mashambulizi yoyote ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran

Zaidi ya ndege 300 zisizo na rubani na makombora zilirushwa Israel usiku kucha, Iran ilisema ni kujibu shambulio la Aprili 1 dhidi ya ubalozi wake nchini Syria.

Muhtasari

• Takriban silaha zote zilidunguliwa na majeshi ya Israel, Marekani na washirika kabla ya kufikia malengo yao.

Rais wa Marekani Joe Biden amsihi Benjamin Netanyahu kujizuia la sivyo 'abebe msalaba wake yenyewe'
Rais wa Marekani Joe Biden amsihi Benjamin Netanyahu kujizuia la sivyo 'abebe msalaba wake yenyewe'
Image: Reuters

Ikulu ya White House imeionya Israel kwamba Marekani haitashiriki katika mashambulizi yoyote ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran, maafisa wakuu wa utawala wamesema.

Zaidi ya ndege 300 zisizo na rubani na makombora zilirushwa Israel usiku kucha, jambo ambalo Iran ilisema ni kujibu shambulio la Aprili 1 dhidi ya ubalozi wake nchini Syria.

Takriban silaha zote zilidunguliwa na majeshi ya Israel, Marekani na washirika kabla ya kufikia malengo yao.

Maafisa walisema Joe Biden aliitaka Israeli kuzingatia majibu yake "kwa uangalifu".

Akizungumza na waandishi habari siku ya Jumapili, afisa mkuu wa utawala alisema kuwa Bw Biden alimwambia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu "kufikiri kwa makini sana na kuweka mikakati" kuhusu jinsi vikosi vyake vitajibu hatua hiyo ambayo haijawahi kushuhudiwa, shambulio la kwanza la moja kwa moja lililofanywa na Iran nchini humo.

Afisa huyo aliongeza kuwa utawala wa Biden unaamini kuwa Israel "ilipata kilicho bora zaidi" katika mgogoro huo, ambao ulianza wakati makamanda wakuu wa jeshi la Iran walipouawa katika jengo la ubalozi wa Iran nchini Syria.

Takriban 99% ya makombora, ndege zisizo na rubani na makombora ya baharini yaliyorushwa wakati wa operesheni ya kulipiza kisasi ya Iran yalidunguliwa au kunaswa - jambo ambalo maafisa wa Marekani wanaashiria kuwa ni ishara ya ukuu wa kijeshi wa Israel dhidi ya Iran.

Ndege za Marekani na vyombo vya majini vilidungua makumi ya makombora ya Iran wakati shambulio hilo likifanyika. Zaidi ya ndege zisizo na rubani 80 na angalau makombora sita yalitunguliwa na ndege na vyombo vya maji vya Marekani au na vikosi vya ulinzi wa anga huko Iraq.

Hii ni pamoja na ndege saba zisizo na rubani na kombora la balestiki walipokuwa wakijiandaa kurusha kutoka Yemen, Afisi Kuu ya kijeshi Marekani (Centcom) iliongezea katika taarifa ya siku ya Jumapili.

Mazungumzo yalifanyika kati ya Bw Biden na Bw Netanyahu wakati "ya hisia kali" baada tu ya shambulio hilo, ambalo lilijumuisha takriban makombora 100 ya balestiki yaliorushwa kwa wakati mmoja kuelekea Israel.