Helikopta mbili za jeshi la wanamaji zagongana angani na kuua wanajeshi 10

"Wahasiriwa wote walithibitishwa kufariki katika eneo la tukio na kupelekwa katika hospitali ya kijeshi ya kituo cha jeshi la majini ili kutambuliwa," jeshi la wanamaji lilisema.

Muhtasari

• Tukio hilo lilitokea katika kituo cha wanamaji cha Lumut katika jimbo la magharibi la Perak saa 9.32 asubuhi ya Jumanne jeshi la wanamaji lilisema.

Helikopta mbili za jeshi la wanamaji la Malaysia ziligongana angani wakati wa mazoezi ya gwaride la wanamaji siku ya Jumanne, na kuua wafanyakazi wote 10 waliokuwa ndani, jeshi la wanamaji la nchi hiyo lilisema katika taarifa.

Tukio hilo lilitokea katika kituo cha wanamaji cha Lumut katika jimbo la magharibi la Perak saa 9.32 asubuhi ya Jumanne jeshi la wanamaji lilisema.

"Wahasiriwa wote walithibitishwa kufariki katika eneo la tukio na kupelekwa katika hospitali ya kijeshi ya kituo cha jeshi la majini cha Lumut ili kutambuliwa," jeshi la wanamaji lilisema.

Video iliyosambaa kwenye vyombo vya habari vya ndani ilionyesha helikopta kadhaa zikiruka kwa mpangilio, wakati rota moja ya chopper ilipokata nyingine kabla ya ndege zote mbili kuanguka ardhini. Polisi wa eneo hilo walithibitisha kuwa picha hizo zilikuwa za kweli.

Jeshi la wanamaji limesema litafanya uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Waziri wa Ulinzi Mohamed Khaled Nordin alisema ndege hiyo - helikopta ya shughuli za baharini na chopa ya kijeshi ya Fennec - walikuwa wakifanya mazoezi ya gwaride la kuadhimisha miaka 90 ya Jeshi la Wanamaji la Kifalme la Malaysia, linalopaswa kufanywa Jumamosi.

Taarifa hizi zinajiri siku chache baada ya helikopta mbili za kijeshi nchini Japan kugongana angani pia katika tukio ambalo liligharimu maisha ya mtu mmoja na wengine 7 kujeruhiwa vibaya.

Mwishoni mwa wiki jana pia, taifa la Kenya lilitupwa katika kipindi cha maombolezo baada ya helikopta ya kijeshi kuanguka mpakani mwa kaunti ya Elgeyo Marakwet na West pokot.

Ndege hiyo ilikuwa imewabeba wanajeshi Zaidi ya 10, miongoni mwao akiwa mkuu wa majeshi ya ulinzi, Francis Ogolla ambaye aliangamia katika ajali hiyo.

Ogolla alizikwa Jumapili nyumbani kwake kaunti ya Siaya, ndani ya saa 72 kufuatia kifo chake kulingana na wosia aliouacha.