China yashukiwa kudukua taarifa za mishahara ya wanajeshi wa Uingereza

Serikali ya Uingereza inashuku China ilihusika na udukuzi wa mfumo wa malipo wa vikosi vya jeshi.

Muhtasari

•Mfumo unaotumiwa na Wizara ya Ulinzi (MoD) unajumuisha majina na maelezo ya benki ya wafanyakazi wa jeshi. 

•Serikali ilifahamu kuhusu udukuaji wa data katika siku za hivi karibuni, na haijapata ushahidi wa wadukuzi

Image: BBC

Serikali ya Uingereza inashuku China ilihusika na udukuzi wa mfumo wa malipo wa vikosi vya jeshi, BBC imefahamu.

Waziri wa Ulinzi Grant Shapps hatataja waliotekeleza uhalifu huo atakapowahutubia wabunge leo, lakini anatarajiwa kuonya juu ya hatari inayoletwa na ujasusi wa mtandao kutoka kwa mataifa hasimu.

Mfumo unaotumiwa na Wizara ya Ulinzi (MoD) unajumuisha majina na maelezo ya benki ya wafanyakazi wa jeshi. China ilisema "inapinga aina zote za mashambulizi ya mtandao".

Katika idadi ndogo sana ya matukio, data inaweza kujumuisha anuani za binafsi.

Mfumo huo, ulio na "taarifa za binafsi za mamlaka ya kodi, HMRC" kwa wanachama wa sasa na wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Kifalme, Jeshi la anga kipindi cha miaka kadhaa, ulisimamiwa na mkandarasi wa nje.

Serikali ilifahamu kuhusu udukuaji wa data katika siku za hivi karibuni, na haijapata ushahidi wa wadukuzi walioondoa data kwenye mfumo.

Waziri wa Baraza la Mawaziri Mel Stride aliiambia Sky News serikali inachukulia usalama wa mtandao "kwa uzito mkubwa" na kuchukua hatua "haraka sana".

Vyanzo vya habari vimeiambia BBC kwamba uchunguzi wa ni nani alihusika na tukio hilo, ambao utaonekana kuwa wa aibu kwa MoD, uko katika hatua ya awali.

Inaweza kuchukua miezi, wakati mwingine miaka, kukusanya ushahidi wa kutosha.