Rais wa Iran ahofiwa kufariki katika ajali ya ndege

Vyombo vya habari vya serikali vinasema Rais Ebrahim Raisi alikuwa kwenye helikopta iliyotua kwa shida Jumapili.

Muhtasari

•'Hakuna dalili za yeyote aliye hai' katika eneo la ajali ya helikopta ya raisi wa Iran Ebrahim Raisi- TV ya serikali imesema.

•Rais Raisi alikuwa akielekea katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, baada ya kurejea mpakani na Azerbaijan.

Rais wa Iran Ebrahim Raisi
Image: BBC

"Hakuna dalili" za yeyote aliye hai katika helikopta iliyombeba Rais Ebrahim Raisi, TV ya serikali inasema.

Shirika la habari la Reuters pia limeripoti kuwa helikopta hiyo "iliungua kabisa" katika ajali hiyo, ikimnukuu afisa wa Iran.

Helikopta iliyombeba rais wa Iran ilihusika katika ajali siku ya Jumapili, vyombo vya habari vya serikali viliripoti.

Vyombo vya habari vya serikali vinasema Rais Ebrahim Raisi alikuwa kwenye helikopta ambayo ilitua kwa shida siku ya Jumapili.

Pia ilisemekana kumbeba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian.Waziri wa Mambo ya Ndani alisema waokoaji bado wanajaribu kufika eneo hilo kutokana na hali ngumu ya hewa.Hali ya waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo bado haijajulikana kwa sasa, huku ripoti kuwa bado hakuna mawasiliano yaliyofanywa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Rais Raisi alikuwa akielekea katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, baada ya kurejea mpakani na Azerbaijan, ambako alifungua mabwawa ya Qiz Qalasi na Khodaafarin.

Ukungu mkubwa ulifanya msako kuwa mgumu katika eneo ambalo inadhaniwa kuwa huenda helikopta hiyo ilitua, kulingana na ripota wa shirika la habari la Fars.

Alisema mwonekano katika eneo la milima na misitu ulikuwa chini hadi takriban mita tano tu.Eneo hilo ni kama kilomita 50 kaskazini mwa Tabriz.

Ahmad Alirezabeigi, Mbunge wa Iran katika mji wa Tabriz amewaambia waandishi wa habari mjini Tehran kwamba waokoaji bado hawajapata eneo la helikopta iliyombeba rais na waziri wa mambo ya nje.

Aliongeza kuwa helikopta nyingine mbili katika msafara huo zilitua salama.Kanda za video zimeibuka kwenye televisheni ya taifa zikionyesha waumini wakimuombea afya rais katika mji mtakatifu wa Mashhad.

Rais wa Iran Ebrahim Raisi ni nani?

Bw Raisi, 63, alichaguliwa kuwa rais katika jaribio lake la pili mwaka wa 2021.

Anaonekana kama mhubiri mwenye msimamo mkali na anachukuliwa kuwa mrithi wa Ayatollah Khamenei siku moja, kiongozi mkuu wa nchi hiyo tangu 1989.

Mnamo mwaka wa 2019, Kiongozi Mkuu alimteua kwenye nafasi yenye nguvu ya mkuu wa mahakama.

Bw Raisi pia alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa Bunge la Wataalamu, baraza la makasisi lenye wanachama 88 walio na jukumu la kumchagua Kiongozi Mkuu ajaye.