Waganda 23 waliotekwa Myanmar 2023 warudishwa nyumbani

Serikali ya Uganda ilianzisha mazungumzo ya kidiplomasia na serikali ya Myanmar ili kuwaachilia raia hao

Muhtasari

•23 hao wamerejea nyumbani kwa kulakiwa kwa fivijo na nderemo kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe nchini humo.

•Serikali ya Uganda imeahidi kuwahamisha raia wengine wanaozuiliwa kwenye nchi za kigeni

Raia wa Uganda kwenye uwanja wa Kimataifa wa ndege Entebbe
Raia wa Uganda kwenye uwanja wa Kimataifa wa ndege Entebbe

Raia  wa Uganda waliokuwa wameshikwa mateka nchini Myanmar wamerejea nyumbani kwa kulakiwa kwa fivijo na nderemo kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe nchini humo.

Kundi hilo, lenye idadi ya watu 23  lilipokelewa na maafisa wa serikali baada ya kuwasili ndani ya mashirika ya ndege ya Ethiopia mwendo wa saa tano asubuhi Alhamisi. Bw Vincent Bagiire Waiswa, katibu mkuu wizara ya mashauri ya kigeni alikaribisha kundi hilo lakini akawaonya Waganda kujihadhari na miradi ya ulaghai ya ajira nje ya nchi.

“Suala hili lilidhihirika mwaka wa 2023 wakati ripoti zilipoibuka kuhusu Waganda 23 waliokuwa wakishikiliwa huko Tachileik, Myanmar, baada ya kushawishiwa na ahadi za kazi zenye malipo makubwa. Baadaye walilazimishwa kuingia katika ulaghai wa kutumia sarafu ya crypto na kusafirishwa kwa magendo kuvuka mipaka,” Bwana Bagiire alisema.

Aliongeza, "Serikali ya Uganda, kwa kushirikiana na Kamisheni Kuu ya Uganda huko Kuala Lumpur, wizara ya mambo ya ndani, na ofisi ya waziri mkuu, ilianzisha mfululizo wa mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Myanmar, na kusababisha makubaliano kuwaachilia Waganda.”

Kulingana na Bw.Bagiire, kufuatia kuachiliwa kwao, kundi hilo lilihifadhiwa katika mpaka wa Thailand na Myanmar, kwa usaidizi wa serikali ya Thailand na shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM).

Balozi wa Uganda nchini Thailand Bi.Betty Bigombe alisema wanafanya juhudi kuwarejesha makwao Waganda zaidi ambao bado wamekwama Myanmar.

“Kambi zipo nyingi, moja inaitwa UK, ya mwisho walikuwa Mlimani ambako walipigwa na nguvu za umeme. Bado tuna Waganda wawili nchini Uingereza na 12 au 13 huko Mlimani.Hatuna uhakika kama kuna wengine wengi,” Bi Bigombe alisema.

 Bigombe alisema kuna haja ya kutafuta suluhu la kudumu kwa visa vinavyoongezeka vya ulanguzi wa binadamu kusini mashariki mwa Asia.

"Kuna zaidi ya watu 100,000 kutoka duniani kote hasa kutoka nchi maskini zinazoendelea ambao wanalengwa hasa vijana kwa sababu ya ukosefu wa ajira," alisema.

Mkuu wa misheni wa shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM) Bw.Sanusi Tejan Savage alisema waliorejea ambao ni pamoja na wanawake watano na wanaume 18 watapata ukarabati kwa mwezi mmoja kabla ya kurejeshwa nyumbani, ili kuunganishwa na familia zao.