Papua New Guinea yahofia maelfu ya watu wamefukiwa baada ya maporomoko ya ardhi

Kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Maafa nchini humo alisema katika barua yake inahofiwa zaidi ya watu 2,000 walizikwa wakiwa hai katika maafa ya Ijumaa.

Muhtasari
  • Chini ya miili 12 imepatikana kufikia sasa, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukikadiria idadi ya waliopotea kuwa 670.
Papua New Guinea yahofia maelfu ya watu wamefukiwa baada ya maporomoko ya ardhi
Image: REUTERS

Kuna hofu kwamba idadi ya watu waliopotea kufuatia maporomoko ya udongo huko Papua New Guinea huenda ikafikia maelfu, shirika la serikali limesema.

Kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Maafa nchini humo alisema katika barua yake inahofiwa zaidi ya watu 2,000 walizikwa wakiwa hai katika maafa ya Ijumaa.

Hata hivyo, idadi kamili ya majeruhi imekuwa vigumu kubainisha na makadirio yametofautiana sana, kwani juhudi za uokoaji zimezuiwa na kifusi cha kina cha mita 10 (futi 32) katika baadhi ya maeneo na ukosefu wa vifaa vya kutosha.

Chini ya miili 12 imepatikana kufikia sasa, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukikadiria idadi ya waliopotea kuwa 670.

Kuporomoka kwa upande wa mlima mapema Ijumaa asubuhi kuliangamiza kijiji chenye shughuli nyingi katika jimbo la Enga, na uharibifu ukiendelea kwa karibu kilomita moja, waangalizi wanaripoti.

Takriban watu 3,800 walikuwa wakiishi katika eneo hilo kabla ya maafa hayo.

Barua hiyo ya Lusete Laso Mana ilisema uharibifu huo ni "mkubwa", na kwamba "umesababisha athari kubwa katika maisha ya kiuchumi ya nchi".

Waziri Mkuu James Marape ametoa rambirambi zake na kuamuru jeshi la ulinzi la nchi hiyo na mashirika ya dharura kufika eneo hilo, takriban kilomita 600 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu Port Moresby.

Lakini wenyeji katika kijiji cha Kaokalam kilichoathiriwa wanasema bado wanasubiri maafisa kuingilia kati na operesheni ya uokoaji.

Mkazi mmoja, Evit Kambu, alisema anaamini wengi wa wanafamilia wake walikuwa wamenaswa chini ya vifusi.

"Nina jamaa zangu a18 waliofukiwa chini ya vifusi na udongo ambao nimesimama juu yake. Wanakijiji walioathiriwa ni wengi sana siwezi kuwahesabu," aliambia shirika la habari la Reuters.