Video ya waziri kuhusu adhabu dhidi ya wapenzi wa jinsi moja yazua gumzo

''Mapenzi kati ya baba na baba, mama na mama, utafungwa miaka mitano hadi kumi na tano jela

Muhtasari
  • Katika video hiyo Waziri Constant Mutamba anaonekana akiahidi kuidhinisha kifungo cha kati ya miaka mitano hadi kumi na tano na faini ya pesa milioni 30 franga za Congo. Takriban dola za Kimarekani 10,000.
Mwanaharakati akipeperusha bendera ya kujivunia mashoga wakati wa maandamano huko Nairobi. Picha: MAKTABA
Mwanaharakati akipeperusha bendera ya kujivunia mashoga wakati wa maandamano huko Nairobi. Picha: MAKTABA

Video kuhusu adhabu dhidi ya wapenzi wa jinsi moja iliyotoleawa na waziri mpya wa sheria aliyeteuliwa wiki hii imeibua gumzo nchini DRC hususan miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo.

Katika video hiyo Waziri Constant Mutamba anaonekana akiahidi kuidhinisha kifungo cha kati ya miaka mitano hadi kumi na tano na faini ya pesa milioni 30 franga za Congo. Takriban dola za Kimarekani 10,000.

''Mapenzi kati ya baba na baba, mama na mama, utafungwa miaka mitano hadi kumi na tano jela, mambo haya yanapaswa kumalizika, utalipa faini ya milioni 30 pesa za Congo'' anasema Constant Mutamba katika video hiyo iliosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza na BBC, waziri huyu wa sheria, amesema, video hii ilirekodiwa mwezi moja kabla uteuzi wake kama waziri, na ni mswada wa sheria ambao aliwasilisha bungeni baada ya kuchaguliwa kama mbuge na kuteuliwa kuwa waziri na hatua hiyo haitamzuia kuendeelea na mswada huo.

''Video hiyo kweli ni yangu ilirekodiwa mwezi moja kabla kuteuliwa kwangu, lakini nimewahakikishia ya kwamba hiyo ni moja ya vipaumbele vyangu, ni moja ya mswada wangu wa sheria'' na nitaendelea kufuatilia, mapenzi ya jinsia moja hayawezi kamwe kukubaliwa Katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo’’ amesisitiza Constant Mutamba Tungulu, ambae ni waziri mpya wa sheria.