Watu wanane wafariki dunia huku India ikikabiliwa na wimbi la joto kali

Mnamo tarehe 31 Mei, watu wasiopungua 33, wakiwemo maafisa wa uchaguzi, walifariki dunia kwa joto kali huko Bihar, Uttar Pradesh na Odisha.

Muhtasari
  • Takwimu rasmi zilizotolewa Mei zilipendekeza watu 60 walifariki dunia kati ya Machi na Mei kote India kutokana na magonjwa yanayohusiana na joto.
Image: BBC

Joto kali linaendelea kusababisha maafa nchini India huku jimbo la mashariki la Odisha siku ya Jumatatu liliporipoti vifo vinane ndani ya kipindi cha saa 72.

Takwimu rasmi zilizotolewa Mei zilipendekeza watu 60 walifariki dunia kati ya Machi na Mei kote India kutokana na magonjwa yanayohusiana na joto.

Lakini idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kwani vifo vinavyotokana na joto haviripotiwi sana katika maeneo ya vijijini.

Maafisa wanasema India iko katikati ya wimbi refu zaidi la joto kuwahi kutokea tangu rekodi kuanza. Halijoto imevuka selsiasi 50 katika baadhi ya maeneo hivi karibuni.

"Hii imekuwa kipindi kirefu zaidi kwa sababu imeshuhudiwa kwa takriban siku 24 katika maeneo mbalimbali ya nchi," Mrutyunjay Mohapatra wa Idara ya Hali ya Hewa ya India (IMD) aliliambia gazeti la Indian Express.

Sehemu za kaskazini mwa India zimekuwa zikishuhudia joto kali tangu katikati ya Mei, huku halijoto ikitanda kati ya selsiasi 45-50 katika miji kadhaa.

Baadhi ya maeneo ya nchi pia yameathiriwa na uhaba wa maji.

Mapema mwezi huu, maafisa wasiopungua 18 waliotumwa kwa awamu ya mwisho ya uchaguzi mkuu walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na joto katika majimbo ya Uttar Pradesh na Bihar, mamlaka ilisema.

Mnamo tarehe 31 Mei, watu wasiopungua 33, wakiwemo maafisa wa uchaguzi, walifariki dunia kwa joto kali huko Bihar, Uttar Pradesh na Odisha.