Putin aweka masharti yake ya kusitisha mapigano nchini Ukraine

Rais wa Urusi pia alisema Ukraine italazimika kukata tamaa kujiunga na Nato kabla ya mazungumzo ya amani kuanza.

Muhtasari

•Putin amesema Ukraine itahitaji kuondoa kikamilifu wanajeshi wake katika maeneo ambayo Urusi inadai kuwa imetwaa kabla ya kuanza kwa usitishaji mapigano.

Rais wa Russia Vladmir Putin
Image: BBC

Vladimir Putin amesema Ukraine itahitaji kuondoa kikamilifu wanajeshi wake katika maeneo ambayo Urusi inadai kuwa imetwaa kabla ya kuanza kwa usitishaji mapigano - pendekezo ambalo Ukraine ililitajamara mojakama "hatua inayokera fikra za kawaida".

Rais wake, Volodymyr Zelensky, amesema kwa muda mrefu Ukraine haitafanya mazungumzo na Moscow hadi pale majeshi ya Urusi yatakapoondoka katika maeneo yote ya Ukraine, ikiwemo Crimea.

Rais wa Urusi pia alisema Ukraine italazimika kukata tamaa kujiunga na Nato kabla ya mazungumzo ya amani kuanza.

Kauli ya Bw Putin inayoweka masharti yake ya kusitisha mapigano inakuja wakati viongozi kutoka mataifa 90 wakijiandaa kukutana nchini Uswizi siku ya Jumamosi kujadili njia za kuelekea amani nchini Ukraine - mkutano ambao Urusi haijaalikwa.

Akizungumza kwenye mkutano wa mabalozi wa Urusi mjini Moscow siku ya Ijumaa, Bw Putin alitoa wito kwa serikali ya Ukraine kujiondoa katika mikoa minne inayokaliwa kwa sehemu na Urusi - Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia.

Pia alisema Ukraine itahitaji kujitoa rasmi katika juhudi zake za kujiunga na muungano wa kijeshi wa Nato ili Urusi ikomeshe jitihada zake za kuendelea kuyatwa maeneo zaidi .

Bw Putin alisema: "Mara tu Kyiv itakapotangaza kuwa iko tayari kwa uamuzi kama huo ... amri ya kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo itafuata mara moja kutoka kwa upande wetu, kwa dakika moja."

Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak alitaja pendekezo hilo kuwa "uzushi kamili"

Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema: "Ni upuuzi kwa Putin, ambaye alipanga, kuandaa na kutekeleza, pamoja na washirika wake, uvamizi mkubwa zaidi wa kutumia silaha barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia, kujionyesha kama mpenda amani."