Mazungumzo ya amani yatafanyika iwapo Urusi itaondoka Ukraine - Zelensky

Hati ya mwisho ilipitishwa ambayo ililaumu Urusi kwa mateso na uharibifu mkubwa wa vita.

Muhtasari
  • Lakini akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano wa kilele wa amani nchini Uswisi, alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin hatamaliza vita hivyo inabidi azuiwe "kwa njia yoyote ile tunayoweza", iwe kwa njia za kijeshi au za kidiplomasia.

Kyiv itafanya mazungumzo ya amani na Urusi  ikiwa Moscow itajiondoa kutoka kwenye ardhi yote ya Ukraine, Rais Volodymyr Zelensky amesema.

Lakini akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano wa kilele wa amani nchini Uswisi, alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin hatamaliza vita hivyo inabidi azuiwe "kwa njia yoyote ile tunayoweza", iwe kwa njia za kijeshi au za kidiplomasia.

Misaada ya nchi za Magharibi haikutosha kushinda vita hivyo, aliongeza, lakini mkutano huo umeonesha kuwa uungwaji mkono wa kimataifa kwa Ukraine haukudhoofika.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa nchi kadhaa kujitolea kudumisha uadilifu wa eneo la Ukraine.

Hati ya mwisho ilipitishwa ambayo ililaumu Urusi kwa mateso na uharibifu mkubwa wa vita.

Hata hivyo, nchi kadhaa zilizohudhuria zikiwemo India, Afrika Kusini na Saudi Arabia hazikutia saini. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuunda uungaji mkono mpana zaidi kwa mchakato ambao unaweza kusaidia kumaliza vita nchini Ukraine.

Zaidi ya nchi 90 na mashirika ya kimataifa walihudhuria mkutano huo. Urusi haikualikwa, na mfadhili wake mkuu China hakuwepo, na hivyo kusababisha baadhi ya watu kutilia shaka ufanisi wa mkutano huo.

Bw Zelensky aliwashukuru viongozi wa dunia waliohudhuria, akisema anashukuru kwamba wameonesha uhuru wao kuja licha ya shinikizo kutoka kwa Urusi kuwataka kukaa mbali. "Mkutano huu unasema kwamba uungwaji mkono wa kimataifa [kwa Ukraine] haudhoofu," alisema, akibainisha kuwa mataifa ambayo hapo awali hayakushiriki katika juhudi za kidiplomasia yalikuwa yamejiunga na mchakato huo.