Waombolezaji wafariki kwa ajali ya gari katika msafara wa mazishi wa Makamu wa Rais wa Malawi

Katika ghasia hizo, gari moja lilitoka nje ya barabara na kugonga makundi ya waombolezaji na kuwaua wanne kati yao

Muhtasari
  • Maelfu ya watu walikuwa wamejipanga barabarani ili kuona jeneza hilo lilipokuwa likisafirishwa kwa maziko siku ya Jumapili.

Watu wanne, akiwemo mwanamke mjamzito, wamepoteza maisha baada ya gari lililokuwa kwenye msafara uliokuwa umebeba mwili wa marehemu Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima kuwagonga waombolezaji, polisi walisema.

Watu wengine kumi na wawili walijeruhiwa katika tukio hilo la Jumapili usiku na walikuwa wakipatiwa matibabu hospitalini.

Ilifuatia mapigano kati ya wenyeji, polisi na wanajeshi waliokuwa wakisindikiza msafara wa marehemu makamu wa rais kutoka mji mkuu, Lilongwe, hadi kijijini kwake kwa mazishi.

Bw.Chilima alifariki katika ajali ya ndege wiki moja iliyopita na anatarajiwa kuzikwa baadaye Jumatatu katika wilaya ya nyumbani kwake Ntcheu, kilomita 180 (maili 112) kusini mwa mji mkuu.

Maelfu ya watu walikuwa wamejipanga barabarani ili kuona jeneza hilo lilipokuwa likisafirishwa kwa maziko siku ya Jumapili.

Msafara huo ulipopita maeneo ya karibu na nyumbani kwa Bw Chilima, baadhi ya watu walianza kurushia mawe magari ya serikali na viongozi.

Katika ghasia hizo, gari moja lilitoka nje ya barabara na kugonga makundi ya waombolezaji na kuwaua wanne kati yao, kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Msemaji wa chama cha UTM cha Bw Chilima aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kulikuwa na hali ya wasiwasi njiani huku waombolezaji wakitaka msafara huo usimame ili waweze kuona jeneza.

"Huko Dedza, watu walifunga barabara na kutaka kuona jeneza," Felix Njawala alinukuliwa akisema. Msafara uliendelea baada ya waombolezaji kutulia.