Bunge nchini Gambia lapinga mswada wa kuruhusu ukeketaji

Spika wa Bunge, Fabakary Tombong Jatta alisema wabunge wengi wamepiga kura dhidi ya mswada huo.

Muhtasari

•Wabunge nchini Gambia wamekataa mswada unaotaka kubatilisha marufuku ya mwaka 2015 ya ukeketaji wa wanawake (FGM).

Image: BBC

Wabunge nchini Gambia wamekataa mswada unaotaka kubatilisha marufuku ya mwaka 2015 ya ukeketaji wa wanawake (FGM).

Spika wa Bunge, Fabakary Tombong Jatta alisema wabunge wengi wamepiga kura dhidi ya mswada huo hata kabla ya kusomwa kwa mara ya tatu na mwisho, unaotarajiwa baadaye mwezi huu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa yalikuwa yamewataka wabunge kuzuia mswada huo uliowasilishwa mwezi Machi baada ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu.

Gambia ni miongoni mwa nchi 10 zenye viwango vya juu vya ukeketaji, huku asilimia 73 ya wanawake na wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wakiwa wamefanyiwa utaratibu huo.

Rasimu ya sheria, iliyowasilishwa na Almameh Gibba, ilikataliwa baada ya wabunge kupiga kura dhidi ya vifungu vyake vyote vilivyopendekezwa.

Bi Jatta alisema mswada huo "umekataliwa na mchakato wa kutunga sheria umekamilika", na kwa hivyo haungeweza kwenda hatua iliyofuata yaani kusomwa kwa mara ya tatu.

Ulipowasilishwa mwezi Machi, mswada huo uliidhinishwa na wabunge wengi, na hivyo kuongeza matarajio ya Gambia kuwa nchi ya kwanza kubatilisha marufuku ya tabia hiyo.

Katika utaratibu wa ukeketaji, baada ya kuondoa sehemu nyeti ‘’kisimi’’, sehemu za siri hukatwa na kushonwa kwa karibu ili mwanamke asiweze kufanya au kufurahiya tendo la ndoa.