Polisi wapiga marufuku maandamano yanayoratibiwa kuelekea bungeni nchini Uganda

Maandamano hayo yaliyokuwa yamepangwa yalikuwa yamechukua mvuto mkubwa, hasa baada ya Waziri wa Fedha anayeshughulikia Uwekezaji na Ubinafsishaji, Evelyn Anite, kuonyesha nia yake ya kushiriki.

Muhtasari

• Uamuzi huo unakuja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka na juhudi kubwa za uhamasishaji kwenye mitandao ya kijamii zinazolenga kupata ushiriki wa umma kwa hafla hiyo.

• ACP Kituuma Rosoke, katika taarifa yake, alisisitiza kukosekana kwa uwazi kuhusiana na maelezo ya waandalizi wa maandamano hayo.

 

Polisi wa Uganda wametangaza kughairi zoezi lililokuwa likitarajiwa kuwa la vijana nchini humo kuandamana kuelekea katika majengo ya bunge wakilaani ufisadi.

Maandamano hayo yanataajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu.

Tangazo la kuyapiga marufuku maandamano ya aina hiyo lilitolewa Jumatatu asubuhi na Msemaji wa Polisi wa Uganda, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kituuma Rosoke kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.

Uamuzi huo unakuja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka na juhudi kubwa za uhamasishaji kwenye mitandao ya kijamii zinazolenga kupata ushiriki wa umma kwa hafla hiyo.

ACP Kituuma Rosoke, katika taarifa yake, alisisitiza kukosekana kwa uwazi kuhusiana na maelezo ya waandalizi wa maandamano hayo.

"Polisi wa Uganda wanataarifiwa kuhusu juhudi zinazoendelea za uhamasishaji kwenye mitandao ya kijamii kuwataka watu kuandamana hadi bungeni. Waandaaji wasiojulikana wamesambaza mabango ya kuwataka watu kukusanyika katika mitaa yote ya Kampala Jumanne, Julai 23, 2024, lakini wakati wa kuanza na maelezo ya shirika havieleweki," Rosoke alisema.

Alisema kuwa utata huu unaweza kusababisha machafuko yanayoweza kutokea.

Msemaji huyo wa polisi alionya zaidi dhidi ya kuendelea na maandamano hayo, akisisitiza umuhimu wa kudumisha utulivu wa umma.

"Kutokana na kukosekana kwa uwazi na uwezekano wa kutokea kwa fujo, polisi wanaonya vikali dhidi ya kuendelea na maandamano haya. Jeshi la Polisi la Uganda linatoa onyo la wazi dhidi ya majaribio ya kuchochea ghasia au uvunjaji wa utaratibu wa umma kupitia maandamano yasiyodhibitiwa," alisema.

Ingawa haki ya maandamano ya amani inakubaliwa, polisi walisisitiza kutovumilia kwao vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea ghasia za umma.

Maandamano hayo yaliyokuwa yamepangwa yalikuwa yamechukua mvuto mkubwa, hasa baada ya Waziri wa Fedha anayeshughulikia Uwekezaji na Ubinafsishaji, Evelyn Anite, kuonyesha nia yake ya kushiriki.

Anite, anayejulikana kwa msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi, alikuwa amekubali mwaliko wa mtandaoni wa kujiunga na maandamano.

Katika majibu yake kwenye mitandao ya kijamii, alithibitisha kujitolea kwake kwa kusema, "Niko ndani," na "ndio" alipoulizwa kama atahudhuria maandamano.