Zaidi ya watu 50 wauawa katika maandamano ya kupinga serikali Bangladesh

Polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji katika maeneo kadhaa.

Muhtasari

•Machafuko hayo yanakuja huku viongozi wa wanafunzi wakitangaza kampeni ya kutotii raia kumtaka Waziri Mkuu Sheikh Hasina ajiuzulu.

Image: BBC

Takriban watu 50 wameuawa nchini Bangladesh huku makabiliano kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga serikali yakizidi kuwa mabaya.

Machafuko hayo yanakuja huku viongozi wa wanafunzi wakitangaza kampeni ya kutotii raia kumtaka Waziri Mkuu Sheikh Hasina ajiuzulu.

Polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji katika maeneo kadhaa ya Bangladesh siku ya Jumapili.

Takriban watu 200 wamejeruhiwa. Amri ya kutotoka nje usiku imeanza kutekelezwa huku mamlaka ikijaribu kukomesha maandamano kote nchini.

Maandamano ya wanafunzi yalianza kwa kutaka kukomesha upendeleo katika kazi za utumishi wa umma mwezi uliopita, lakini sasa yamegeuka kuwa vuguvugu kubwa la kupinga serikali.

Siku ya Jumapili Waziri wa Sheria na Haki Anisul Huq aliambia kipindi cha Newshour cha BBC kwamba viongozi wamekuwa "wakijizuia".

“Laiti hatungejizuia kungekuwa na umwagaji damu. Nadhani uvumilivu wetu una mipaka,” aliongeza.

Katika mji mkuu, Dhaka, huduma za intaneti zimefungwa.