Mdahalo kati ya Trump na Harris Kufanyika Septemba

"Tunafikiri tunapaswa kufanya midahalo mitatu," Trump alisema.

Muhtasari

•Trump alisema Alhamisi atakuwa tayari kufanya mdahalo na mpinzani wake wa chama cha Democratic mara nyingi kabla ya uchaguzi wa Novemba.

Image: BBC

Shirika la habari la Marekani ABC News liimesema litaandaa mdahalo wa kwanza kati ya Donald Trump na Kamala Harris tarehe 10 Septemba.

Shirika hilo lilithibitisha mpambano huo katika chapisho kwenye X, zamani ukiitwa Twitter, baada ya Trump kusema Alhamisi kwamba atakuwa tayari kufanya mdahalo na mpinzani wake wa chama cha Democratic mara nyingi kabla ya uchaguzi wa Novemba.

"Tunafikiri tunapaswa kufanya midahalo mitatu," Trump alisema, akipendekeza midahalo miwili ya ziada ambayo alisema itaandaliwa na Fox News na NBC.

Bi Harris alithibitisha kwamba atahudhuria mdahalo wa ABC akiwa kwenye hafla katika jimbo la Michigan siku ya Alhamisi, na akasema baadaye kwamba atakuwa wazi kwa midahalo ya ziada.

ABC News ilisema kuwa mdahalo huo utasimamiwa na mtangazaji mkuu wa kipindi cha World News Tonight David Muir na mtangazaji mkuu wa ABC News Live Linsey Davis.

"Ninatazamia kufanya mdahalo na Donald Trump na tutaufanya tarehe ya Septemba 10. Nasikia hatimaye amejitolea na ninausubiri," Bi Harris alisema katika hafla ya Detroit.

Trump, mgombea wa Republican, alifanya mdahalo na Rais Joe Biden mara moja mwezi Juni.