Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah auawa - Jeshi la Israel

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ameuawa.

Muhtasari

•Katika taarifa iliyoshirikishwa kwenye akaunti ya mtandao wa X ya IDF, inasema: "Hassan Nasrallah hataweza tena kutishia ulimwengu."

Image: BBC

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ameuawa.

Katika taarifa iliyoshirikishwa kwenye akaunti ya mtandao wa X ya IDF, inasema: "Hassan Nasrallah hataweza tena kutishia ulimwengu."

Kauli hiyo inafuatia mfululizo wa mashambulizi ya usiku kucha huko Beirut ambayo Israel ilisema yalikuwa yakimlenga Nasrallah na makamanda wengine wa Hezbollah.

Katika taarifa hiyo, Israel imesema kwamba wanachama wengine waandamizi wa kundi linaloungwa mkono na Iran waliuawa pamoja na Hassan Nasrallah - ikiwa ni pamoja na kamanda wa eneo la kusini la Hezbollah.

IDF inasema ndege za kivita zilifanya "shambulizi lililolengwa" katika makao makuu ya kati ya Hezbollah, ambayo inasema yapo "chini ya ardhi ya jengo la makazi katika eneo la Dahieh huko Beirut".

Inaongeza kuwa shambulizi hilo lilifanyika wakati "makamanda waandimizi" wa kundi hilo walikuwa wakiendeleza shughuli zao kutoka kitongoji cha Dahieh kusini mwa Beirut - ngome ya kundi hilo lenye silaha.

Lakini hadi kufikia sasa, hatujapata maoni yoyote kutoka kwa Hezbollah.

Mkuu wa IDF aapa 'kumfikia' yeyote anayetishia Israel

Mkuu wa Wafanyakazi wa IDF, Lt Jenerali Herzi Halevi, ametuma ujumbe wa video.

"Ujumbe uko wazi sana, yeyote anayetishia raia wa Israel tunajua jinsi ya kuwapata, kaskazini, kusini, au mbali zaidi."

Klipu hii ya video imewekwa kwenye majukwaa ya kijamii ya IDF muda mfupi baada ya kutoa taarifa ikisema kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ameuawa.

Mkuu wa IDF: Kumlenga Nasrallah kulifanyika kwa 'wakati ufaao'

Katika video hiyo iliyohaririwa ya sekunde 52 ya kile kinachoonekana kuwa mkutano wa kutoa taarifa ya kile kinachoendelea pamoja na maafisa wengine wa jeshi.

Luteni Jenerali Herzi Halevi amesema kwamba "mwishowe, baada ya maandalizi mengi", jeshi la Israel "lilianzisha" mpango wao nchini Lebanon wa kumlenga Nasrallah na makao makuu ya Hezbollah katika shambulizi.

"Ilikuwa wakati sahihi, [sisi] tulilifanya kwa njia sahihi mno."

"Huu sio mwisho wa uwezo wetu, tunapaswa kuwa wazi sana. Tuna uwezo zaidi kwenda mbele," Halevi anasema.

Uchambuzi: Israel inazidi kuchukua hatua kali

Madai ya Israel ya kumuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah yataimarisha imani yao kwamba huo ndio ushindi wao mkubwa zaidi dhidi ya adui yao mkubwa.

Wamekusanya wanajeshi zaidi, wanaonekana kutaka kushika kasi na wanaweza hata kufikiria kuhusu uvamizi wa ardhini ndani ya Lebanon.

Ukweli ni kwamba Israel inazidi kuchukua hatua kali.

Katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, kumekuwa na ugomvi unaoendelea kati ya pande zote mbili, ingawa shinikizo zaidi ni kutoka upande wa Israel.

Lakini sasa wameamua watashinikiza zaidi, na watafurahishwa na walichokifanya, kwa sababu, tofauti na vita dhidi ya Hamas, ambavyo hawakutarajia, wamekuwa wakipanga vita hivi tangu 2006 na sasa wanatekeleza mipango yao.

Kuna changamoto kubwa sasa kwa Hezbollah, ikiwa ripoti hii kutoka kwa jeshi la Israel kuhusu kiongozi wa Hezbollah ni kweli au la.

Roketi zao zimekuwa zikitua tena katika eneo la Israeli asubuhi ya leo na kulenga maeneo ya kusini zaidi, kwa hivyo wanarudi nyuma - lakini hiki ni kipindi kisicho na uhakika na hiyo ni sehemu ya hatari.