Ajali ya Treni India: Waziri Mkuu aapa kuwachukulia hatua kali waliohusika

Takriban watu 288 walifariki na wengine takriban 1,000 kujeruhiwa katika ajali hiyo ya Ijumaa jioni.

Muhtasari

•Watu watakaopatikana na hatia ya kuhusiana na ajali mbaya ya reli mashariki mwa India "wataadhibiwa vikali", Waziri Mkuu amesema.

Image: BBC

Watu watakaopatikana na hatia ya kuhusiana na ajali mbaya ya reli mashariki mwa India "wataadhibiwa vikali", Waziri Mkuu wa nchi hiyo Narendra Modi amesema.

Takriban watu 288 walifariki na wengine takriban 1,000 kujeruhiwa katika tukio la Ijumaa jioni katika jimbo la Odisha, lililohusisha treni mbili za abiria na treni ya mizigo.

Juhudi za uokoaji zimekamilika, huku maafisa wakisema abiria wote waliokwama na waliojeruhiwa wamepatikana.

Bw Modi ametembelea eneo la tukio, akitaja tukio hilo kuwa "baya sana".

Pia alikutana na waathiriwa wa ajali hiyo hospitalini, na kuaapa kwamba serikali yake itafanya kila iwezalo "kuwahudumia waliojeruhiwa".

Bado haijabainika ni nini kilisababisha mgongano wa treni hizo katika wilaya ya Balasore, ambayo imeelezwa kuwa ajali mbaya zaidi ya reli nchini India katika karne hii.

Ajali zingine mbaya ya treni nchini India

  • Juni 1981: Watu wapatao 800 walikufa wakati mabehewa saba kati ya tisa ya treni iliyojaa watu yalipoanguka mtoni wakati wa kimbunga.
  • Agosti 1995: Takriban watu 350 waliuawa wakati treni mbili zilipogongana kilomita 200 kutoka Delhi.
  • Agosti 1999: Treni mbili ziligongana karibu na Kolkata na kuua watu wasiopungua 285
  • Oktoba 2005: Watu 77 waliuawa wakati treni ilipotoka katika jimbo la kusini la Andhra Pradesh.
  • Novemba 2016: Takriban watu 150 waliuawa na idadi sawa kujeruhiwa wakati mabehewa 14 ya njia ya treni ya Indore-Patna Express yakiacha njia karibu na mji wa Kanpur.

Article share tools