Uganda: Wanafunzi wa vyuo vikuu wawapongeza wabunge, Museveni kwa sheria kali dhidi ya ushoga

"Mungu Mwenyezi tunaweka mustakabali wetu mikononi mwako, watu tuliounganisha wenye uhuru leo," waliimba

Muhtasari

• Mamia ya wanafunzi waliotoka katika vyuo vikuu 13 kote nchini pia walimshukuru Rais Yoweri Museveni kwa kutia saini Mswada huo kuwa sheria.

•Museveni, mpinzani mkubwa wa haki za mashoga, aliwapongeza wabunge kwa "kukataa shinikizo kutoka kwa mabeberu."

kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini Uganda wakiimba nje ya Bunge la nchi hiyo ambapo walikuwa wameandamana kuwashukuru wabunge kwa kupitisha Mswada wa Kupinga Ushoga na Rais Yoweri Museveni kwa kuuridhia, Mei 31, 2023.
Wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini Uganda wakiimba nje ya Bunge la nchi hiyo ambapo walikuwa wameandamana kuwashukuru wabunge kwa kupitisha Mswada wa Kupinga Ushoga na Rais Yoweri Museveni kwa kuuridhia, Mei 31, 2023.
Image: HISANI

Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Uganda wameandamana hadi Bunge la nchi hiyo mjini Kampala kuwashukuru wabunge kwa kupitisha Mswada wa Kupinga ushoga.

Gazeti la Daily Monitor linaripoti kuwa mamia ya wanafunzi waliotoka katika vyuo vikuu 13 kote nchini pia walimshukuru Rais Yoweri Museveni kwa kutia saini Mswada huo kuwa sheria.

Video zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha wanafunzi hao wakiwa katika maandamano ya amani huku wakiimba nyimbo za kizalendo kuonesha kuwashukuru na kuwa na mshikamano na wabunge na kiongozi wa nchi.

"Mungu Mwenyezi tunaweka mustakabali wetu mikononi mwako, watu tuliounganisha wenye uhuru leo," waliimba kwenye ngazi za mlango wa Bunge.

"Hatutaki pesa zenu zinazounga mkono mashoga. Tunataka na kuipenda nchi yetu zaidi ya pesa," wanafunzi hao walisema.

Museveni siku ya Jumatatu alitia saini kuwa sheria kile kinachojulikana kama Mswada mkali zaidi wa kupinga ushoga duniani ambao unaeleza hukumu ya kifo kwa vitendo vya ushoga.

Ilifuatia kupitishwa kwa Mswada huo kwa wingi na Bunge la Uganda mnamo Machi 21 ambapo ni mbunge mmoja tu kati ya 389 waliohudhuria mjadala huo alipinga kupitishwa kwake.

Museveni, mpinzani mkubwa wa haki za mashoga, aliwapongeza wabunge kwa "kukataa shinikizo kutoka kwa mabeberu."

Sheria inapendekeza adhabu ya kifo kwa ushoga uliokithiri au kulazimisha watoto, walemavu, wagonjwa wa akili na wale walio katika umri mkubwa kufanya ushoga.

Jaribio la kufanya mapenzi ya jinsia moja litavutia kifungo cha miaka 14 jela na hadi miaka 20 kwa kuendeleza ushoga. Waajiri wa watoto wanaofanya mapenzi ya jinsia moja wataadhibiwa kwa kifungo cha miaka kumi jela.

Yeyote ambaye "kwa kujua anaruhusu majengo yao kutumika kwa vitendo vya ushoga" anakabiliwa na kifungo cha miaka saba jela.

Hatua ya Museveni ya kutia saini Mswada huo kuwa sheria iliibua hasira kutoka kwa baadhi ya Waganda na jumuiya ya kimataifa huku Uingereza ikiuita "ubaguzi mkubwa" na ambao "utaharibu sifa ya Uganda kimataifa."

Rais wa Marekani Joe Biden, mtetezi mkubwa wa haki za LGBTQ+, aliitaja kuwa ni "aibu" na "ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu kwa wote."

Alisema Washington inazingatia kuweka "vikwazo na vizuizi vya kuingia Marekani dhidi ya yeyote anayehusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu."

"Ninaungana na watu duniani kote - ikiwa ni pamoja na wengi nchini Uganda - katika kutoa wito wa kufutwa kwake mara moja," Biden alisema.