Wafungwa watoroka kutumia mswaki, wapatikana wakituliza njaa hotelini saa 12 baadaye

Walikamatwa baada ya raia kupiga ripoti baada ya kuwaona katika mkahawa huo.

Muhtasari

• Garza na Nemo walianza kutafutwa baada ya askari jela kugundua hawapo wakati wa kuhesabu wafungwa katika Jela.

•Walikuwa wamechimba shimo kupitia moja ya kuta za jela kwa kutumia zana za kale ambazo walitengeneza kwa kutumia mswaki na chombo cha chuma.

Mfungwa akiwa jela
Mfungwa akiwa jela
Image: Mfungwa Jela

Wafungwa wawili ambao walitoroka katika jela ya Newport News, iliyo katika jimbo la Virginia,  nchini Marekani kwa kuchimba na kukwea ukuta walipatikana katika hoteli ya karibu saa chache baadaye siku ya Jumanne.

Msako wa kuwatafuta wawili hao, John Garza na Arley Nemo, uling'oa nanga mara moja baada ya askari jela kugundua hawapo wakati wa kuhesabu wafungwa katika Jela la Newport News siku ya  Jumatatu usiku.

Ili kufakinikisha kutoroka kwao, wawili hao walikuwa wamechimba shimo kupitia moja ya kuta za jela kwa kutumia zana za kale ambazo walitengeneza kwa kutumia mswaki na chombo cha chuma. Baada ya kutoka nje, walikumbana na kuta zingine za kuzuia na iliwabidi wapande ili kuondoka eneo hilo.

Wafungwa hao walipatikana siku ya Jumanne mwendo wa saa kumi na dakika ishirini asubuhi wakipata kiamsha kinywa katika mkahawa wa IHOP jijini Hampton. Jela ya Newport News iko umbali wa maili sita na nusu kutoka mkahawa huo, safari ya takribani saa mbili na dakika 15 unaposafiri kwa miguu.

Baada ya kupatikana, walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.

Ripoti kutoka Marekani zinasema kwamba Garza na Nemo walikamatwa kufuatia usaidizi wa raia ambao walipiga ripoti baada ya kuwaona katika mkahawa huo

Garza alikuwa amezuiliwa kwa mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupuuza mahakama na kukosa kufika mahakamani. Nemo alikuwa anashikiliwa kwa makosa ya ulaghai wa kadi ya mkopo, kughushi, kupatikana na zana za wizi, kupuuza mahakama na ukiukaji wa muda wa majaribio, kulingana na ofisi ya Sheriff.