Waziri Mkuu wa Uingereza awakashifu vikali wahuni wanaongilia maandamano

“Wale waliohusika na vurugu hizi watakumbana na mkono wa sheria kwa nguvu zote," alisema.

Muhtasari

•Wikendi magenge yalikuwa yakichoma majengo, kushambulia waislamu na watu wa makundi ya makabila mbalimbali, na kukabiliana vikali na polisi.

•Mamlaka baadaye iliweka wazi kwamba mtuhumiwa halisi, kwa jina Axel Rudakubana mwenye umri wa miaka 17, alizaliwa Uingereza lakini vurugu ziliendelea.

Maandamano Uingereza
Image: HISANI

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amekemea vikali vurugu na ghasia za maandamano  yaliyoshuhudiwa katika miji mbalimbali nchini Uingereza.

Wikendi, magenge yalikuwa yakichoma majengo, kushambulia waislamu na watu wa makundi ya makabila mbalimbali, na kukabiliana vikali na polisi.

Akizungumza Jumapili, muda mfupi baada ya waasi kujaribu kuteketeza kwa moto jengo lililokuwa na wahamiaji, Starmer alisema:

“Wale waliohusika na vurugu hizi watakumbana na mkono wa sheria kwa nguvu zote.”

Aliongeza, “Polisi watakuwa wakikamata wahalifu … Nawahakikishia mtajuta washiriki wa machafuko haya. Watu wote wenye akili timamu wanapaswa kulaani aina hii ya vurugu.”

Vurugu hizi zilianza kufuatia taarifa za uongo zilizosambazwa mtandaoni zikidai kwamba mhamiaji Muislamu ndiye alihusika katika shambulio la mauaji lililotokea katika darasa la watoto katika mji wa Southport.

Shambulio hilo, ambalo lilipelekea vifo vya wasichana watatu, lilipotoshwa kwamba lilihusishwa na mhamiaji Muislamu, hali iliyosababisha machafuko makubwa zaidi nchini Uingereza.

Mamlaka baadaye iliweka wazi kwamba mtuhumiwa halisi, kwa jina Axel Rudakubana mwenye umri wa miaka 17, alizaliwa Uingereza lakini vurugu ziliendelea kuchacha zaidi.

Vurugu zimeenea kote Uingereza ikiwemo miji ya Belfast, Bristol, London, na miji mbalimbali katika eneo la midlands na kaskazini mwa Uingereza, kama Blackpool, Hull, Leeds, Manchester, Middlesbrough, Stoke-on-Trent, na Sunderland.

Katika mji wa Rotherham, ambao umekumbwa na hali ya uvunjaji wa sheria na amani kutokana na kashfa za unyanyasaji wa watoto zilizohusisha kundi la wanaume wa Britani-Pakistani mnamo miaka ya 2000, hali ilizidi kuwa mbaya.

Wale waliopinga wahamiaji walivamia hoteli iliyokuwa na wahamiaji, kujaribu kuweka moto kwenye jengo na kuzuia milango.

Polisi walishiriki na kumkamata mmoja wa waasi, huku wakilazimika kuwasogeza nyuma.

Kwa bahati nzuri, hakuna aliyepata majeraha, ingawa wafanyakazi na wenyeji walieleza kuwa “walikuwa na hofu kubwa.”

Vurugu hizo pia zilishuhudia mashambulizi dhidi ya polisi, huku maafisa kumi wakijeruhiwa kwa mujibu wa Sky News.

Waasi hao walijumuisha watoto na baadhi walivaa vikinga uso, mashati ya soka ya England, na kubeba bendera za Uingereza.

Mpiga picha kutoka huduma ya habari ya Ufaransa AFP pia alishambuliwa katika umati huo wakati anachukua picha kwenye kizaazaa hicho.