Kijakazi afungwa miaka 2 kwa kuiba elfu 456,000 za mwajiri wake

Muhtasari
  • Mwendesha mashtaka Ann Wanjiku aliambia mahakama kwamba mshtakiwa alibeba pesa hizo kwenye suti
Mahakama
Mahakama
Image: MAKTABA

Kijakazi amefungwa jela kwa miaka 2 baada ya kukiri shtaka la kuiba pesa za mwajiri wake na kuzipeleka kwa mchungaji bandia wa mtaani.

Faith Ondisa alishtakiwa kwa kuiba Sh456,000 kutoka kwa Mary Mwatika katika eneo la Lavington huko Dagoreti ndani ya kaunti ya Nairobi.

"Yeye (mchungaji) aliniambia kuwa alijua matatizo yangu. Kisha akanishauri ninyooshe mkono wangu, kuupaka mate na kisha akaniambia kuwa kulikuwa na pesa katika nyumba ya mwajiri wangu," Ondisa aliambia mahakama.

Alikubali mashtaka Jumanne mbele ya hakimu wa Kibera William Tulel, lakini aliambia mahakama kwamba alidanganywa na walaghai kando ya Barabara ya Ngong yenye shughuli nyingi.

Mwendesha mashtaka Ann Wanjiku aliambia mahakama kwamba mshtakiwa alibeba pesa hizo kwenye suti.

"Kisha alidanganya walinzi kwamba alikuwa akichukua koti hilo kwa ukarabati," Wanjiku alisema.

Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa mlalamikaji aligundua kuwa mambo hayakuwa sawa baada ya kuwahoji baadhi ya walinzi wa getini ambao walimweleza kuwa mshtakiwa aliondoka kwenye boma hilo akiwa na suti.

Wanjiku pia alisema mshtakiwa alizima simu yake muda mfupi baadaye na kununua laini mpya.

"Alipokagua pesa zake, aligundua kuwa hazipo. Aliwasiliana na mshtakiwa lakini yote hayakufaulu kwani simu yake ilikuwa imezimwa," mwendesha mashtaka alisema.

Mlalamikaji aliamua kuripoti shauri hilo polisi na mshtakiwa alifuatiliwa kwa namba mpya na wapelelezi na kukamatwa.

“Wapelelezi katika kituo cha polisi cha Muthangari walimfuatilia na kumkamata alipokuwa katika nyumba ya mwanamume huko Donholm. Alikiri kuiba pesa hizo na akafikishwa kortini,” Wanjiku alisema.

Tulel alimuamuru kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au amlipe mlalamishi Sh456,000 zake.

Alimpa siku 14 kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ikiwa angetaka kufanya hivyo.