PS wa ugatuzi, Julius Korir ashtakiwa kwa kumdhulumu mkewe mjamzito

Muhtasari

•Julius Korir alifikishwa mahakamani Jumatatu na kushtakiwa kwa kumpiga mkewe aliyekuwa mjamzito, Evelyn Koech. 

•Shitubi alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh20,000. Pia alimuonya  asiwasiliane na mashahidi katika kesi hiyo.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Miundomsingi Julius Korir mbele ya kamati ya Uchukuzi.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Miundomsingi Julius Korir mbele ya kamati ya Uchukuzi.
Image: EZEKIEL AMINGA

Katibu Mkuu katika wizara ya Ugatuzi, Julius Korir alifikishwa mahakamani Jumatatu na kushtakiwa kwa kumpiga mkewe aliyekuwa mjamzito, Evelyn Koech. 

Hii ina maana kwamba anaweza kuondoka kwenye nafasi yake kama PS. 

PS huyo ambaye alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Susan Shitubi, alikanusha mashtaka dhidi yake. 

Karatasi ya mashtaka inasema kuwa mnamo Septemba 17, 2020, katika Barabara ya Ndalat, Karen, jijini Nairobi, mshtakiwa alimpiga Koech na kumdhuru mwili. 

Kupitia kwa wakili wake Nicholas Ombija, mshtakiwa aliomba masharti nafuu ya bondi, akisema hawezi kukimbia kwani yeye ni afisa wa serikali.

Ombija alisema Korir hayuko sawa na kumweka rumande kungezorotesha hali yake. 

"Yeye ndiye anayesimamia Ugatuzi kwa sasa na kuna kongamano linalotarajiwa Mei ambapo washiriki zaidi ya 30,000 kutoka kote bara Afrika wanatarajiwa kuhudhuria.

Kumweka kizuizini kutavuruga kazi ya bara," Ombija aliambia mahakama.

 Upande wa mashtaka haukupinga dhamana yake, bali ulimtaka mshtakiwa kuacha kuwasiliana na mashahidi ambao baadhi yao walikuwa wafanyakazi wake na mlalamikaji walipokuwa wakiishi pamoja. 

Shitubi alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh20,000. Pia alimuonya  asiwasiliane na mashahidi katika kesi hiyo.

 Shitubi aliuelekeza upande wa utetezi kwamba endapo watamaliza kesi hiyo nje ya mahakama, wako huru kurejea tena mahakamani ili kuiondoa kesi hiyo. Kesi hiyo itatajwa Aprili 19.

 Mapema Jumatatu, mahakama ilikuwa imetoa kibali cha kukamatwa kwa PS lakini ikabatilisha baada ya Korir kufika mahakamani. 

DPP asubuhi aliiomba mahakama kutoa hati ya kesi dhidi ya PS kwa kushindwa kuhudhuria mahakamani kwa kesi ya shambulio kwa mara ya tano.

 Korir alitakiwa kufika kortini kuthibitisha iwapo yeye na mkewe waliyeachana naye wamekubali kusuluhisha suala hilo nje ya mahakama. 

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulimweleza hakimu kuwa pande zote hazijafikia makubaliano. 

"Tulitarajia kwamba kesi hiyo ingesuluhishwa leo, lakini kwa kuwa hakuna makubaliano, tunatafuta hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa kwa kuwa yuko nje kwa dhamana ya polisi," mwendesha mashtaka alisema.

 Kupitia kwa wakili wake, Korir aliomba siku saba zaidi kwa suala hilo kusuluhishwa, akisema kuchelewa kulisababishwa na mshtakiwa kuwa na tatizo la uti wa mgongo. 

 "Kilichopunguza kasi ya mchakato huo ni kwamba mshtakiwa ana tatizo na uti wa mgongo. Mfupa mmoja unauma sana na unazuia harakati zake," Ombija aliambia mahakama. 

"Yuko tayari kusuluhisha suala hilo na tunaomba kuja wiki ijayo ili kusuluhisha."

Wakili huyo aliitaka mahakama kutotoa kibali cha kukamatwa wakati kuna juhudi za kusuluhisha mzozo huo zinazoendelea.