Maswali 5 magumu mawakili wa Raila waliulizwa na majaji wa mahakama ya upeo

"Kila uchaguzi ni tofauti, urais, ugavana hadi MCA, je, mgombea wa MCA anaweza kudai kukandamizwa kwa wapiga kura?", Aliuliza.

Muhtasari
  • Maswali 5 magumu mawakili wa Raila waliulizwa na majaji wa mahakama ya upeo
Benchi la majaji saba likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, naibu CJ Lady Justice Philomena Mwilu, Jaji Mohammed Ibrahim, Jaji Dkt. Smokin Wanjala, Lady Justice Njoki Ndungu, Jaji Isaac Lenaola na Jaji William Ouko wakati wa kongamano la kesi kabla ya kuanza kwa ombi la urais katika Mahakama ya Juu Agosti 30, 2022.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Ombi la mwaniaji urais wa muungano wa Azimio Raila Odinga la kutaka kura zibatilishwe liling'oa nanga siku ya Jumatano katika mahakama ya upeo.

Ulifika wakati kwa mawakili wanaowawakilisha walalamishi kutoa mawasilisho yao kwa njia ya mdomo huku timu ya mawakili ya Raila ikiongozwa na James Orengo ikichukua muda kuithibitishia mahakama kuwa uchaguzi wa urais wa Agosti 9 haukuthibitishwa na uwazi.

Baada ya mawasilisho hayo, ilifika zamu ya majaji kuuliza baadhi ya maswali ili kupata ufafanuzi ambapo mawakili hao walilazimika hadi Ijumaa kujibu.

Haya hapa baadhi ya maswali yaliyoulizwa na majaji mbalimbali ambayo ni muhimu katika kutoa maamuzi yao.

Jaji Njoki Ndungu alikuwa na suala na madai kwamba kuahirishwa kwa uchaguzi katika Kakamega na Mombasa kuathiri idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura.

"Kila uchaguzi ni tofauti, urais, ugavana hadi MCA, je, mgombea wa MCA anaweza kudai kukandamizwa kwa wapiga kura?", Aliuliza.

Kwa upande wake jaji Smokin wanjala alishangaa kwa nini makamishna hao wanne walikubali kukabidhiwa majukumu ambayo hayakuwa ndani ya Mamlaka yao.

"Kwa nini makamishna hawakupinga kwamba wanapewa majukumu ambayo hayakuwa ndani ya mamlaka yao?", aliuliza wanjala.

Jaji Mohamed Ibrahim aliwapa kazi Raila Odinga na Martha Karua kuhalalisha ni kwa nini wanataka kutangazwa washindi ikiwa walifaulu.

"Kila ombi litazingatia sheria. Thibitisha msingi wa kikatiba wa maombi ya kuwatangaza Raila na Karua washindi, ikiwa walifaulu", akauliza.

Philomena mwilu: Ni lini IEBC ilishindwa kufanya kazi? Je, ni hatua gani za kurekebisha zilijaribiwa? Isaack Lenaola: Ikiwa Chebukati ataondolewa kama mwenyekiti wa IEBC, je tume hiyo bado itaundwa kisheria?