Jamaa apatikana na hatia ya kumchoma mkewe kwa petroli hadi kufa

Kanini alikuwa amerudi nyumbani kwake pamoja na kakake na rafikiye ili kuchukua nguo zake.

Muhtasari

•Stanley Nduati, alipatikana na hatia ya kumuua mkewe Salome Kanini mnamo Januari 4, 2018 nyumbani kwao eneo la Nkoroi ndani ya Mji wa Ongata Rongai.

•Marehemu alipata asilimia 90 ya majeraha ya moto mwilini mwake na alikimbizwa hospitalini ambapo alifariki.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mahakama kuu mjini Kajiado imempata mwanamume na hatia ya kumuua mkewe kwa kumwagilia petroli na kumchoma moto.

Mshtakiwa, Stanley Nduati, alipatikana na hatia ya kumuua mkewe Salome Kanini mnamo Januari 4, 2018 nyumbani kwao eneo la Nkoroi ndani ya Mji wa Ongata Rongai.

Wanandoa hao walikuwa wametengana kwa mwezi mmoja kwa masuala ya nyumbani na siku hiyo, Kanini alikuwa amerudi nyumbani kwake pamoja na kaka yake na rafiki yake ili kuchukua nguo zake.

Mumewe anaripotiwa kumfungia ndani ya nyumba na hivyo kuwa vigumu kwa kaka yake kumuokoa alipomchoma moto.

Marehemu alipata asilimia 90 ya majeraha ya moto mwilini mwake na alikimbizwa hospitalini ambapo alifariki.

Mshtakiwa alikana kosa la mauaji na alidai kuwa mkewe alichomwa na maziwa ya kuchemsha.

Jaji Stella Mutuku hata hivyo alipuuzilia mbali utetezi wake na kubainisha kuwa ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama umethibitisha bila shaka yoyote kuwa mshtakiwa alimuua mkewe kwa kumwagilia mafuta ambayo yalisababisha mlipuko mkubwa.

"Ushahidi unaonyesha kuwa walipofika mshtakiwa alimvuta marehemu ndani ya nyumba na kufunga mlango na hivyo kutowezekana kwa kaka yake na rafiki yake ambaye alikuwa ameandamana naye kuzuia shambulio dhidi ya marehemu," Mutuku alisema.

Mshtakiwa huyo atahukumiwa baadaye.