Babu Owino alikuwa akivuta shisha kabla ya kumpiga risasi DJ Evolve, mahakama yaarifiwa

Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki yuko mahakamani kwa shtaka la matumizi mabaya ya bunduki.

Muhtasari

•Babu alifika katika kilabu hicho mwendo wa saa tano usiku usiku wa Januari 16, 2020, na kujiunga na watu waliokuwa wakisherehekea.

•Alikuwa ameshtakiwa kwa jaribio la kumua kwa kumpiga risasi DJ Evolve lakini familia hizo mbili zilisuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama.

Babu Owino
Babu Owino
Image: Maktaba

Babu Owino alikuwa akivuta shisha kwa takriban saa sita katika Klabu ya B jijini Nairobi alipompiga risasi DJ Evolve kwenye jumba hilo mnamo Januari 2020, mahakama ilisikiliza Jumatatu.

Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki alifika katika kilabu hicho mwendo wa saa tano usiku usiku wa Januari 16, 2020, na kujiunga watu waliokuwa wakisherehekea huku walinzi wake wakiwa wameketi kwenye kona mbalimbali.

"Alikuwa akijivinjari kwa kuvuta shisha na nilikaa pembeni ambapo niliweza kumuona vizuri," koplo Hamisi Ali alisema.

Afisa huyo wa polisi alihudumu kama mlinzi wa Babu Owino kati ya 2018 na 2020 alipoitwa tena baada ya kisa hicho cha baa.

Hamisi alikuwa na Babu wakati mbunge huyo alipoingia kwenye eneo la burudani na kumlinda hadi saa kumi asubuhi.

Walikuwa walinzi watatu. Wale wengine wawili aliowataja kuwa Walter na Edwin hawakuwa askari polisi.

"Mwendo wa saa kumi asubuhi, Mheshimiwa Babu alituruhudu kwenda na kisha tukaondoka kuelekea nyumbani kwetu," Hamisi alisema.

Na hivyo walinzi waliondoka na Babu akaendelea kujiburudisha pale klabuni.

Flora Charo, mwanamke ambaye alikuwa akisimamia mlango wa klabu hiyo usiku huo, alisema alikumbuka kumuona mbunge huyo akiingia kwenye klabu hiyo akiwa na wanaume wengine.

"Sikumbuki kumuona akiondoka. Kazi yangu ilikuwa ni kuangalia kama wanawake wanaoingia wakiwa wamebeba vinywaji kutoka nje," Charo alisema.

B Club katika eneo la Kilimani ina lango la kuingilia na kutoka, ambayo ina maana kwamba mtu anaweza kuingia na kuondoka bila walinzi wa mlangoni kujua.

Babu Owino alikuwa ameshtakiwa kwa jaribio la kumuua kwa kumpiga risasi DJ Evolve lakini familia hizo mbili zilisuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama.

Mbunge huyo, hata hivyo, yuko mahakamani kwa shtaka la pili la matumizi mabaya ya bunduki.

Hamisi alisema Babu ni kiongozi anayewajibika na hajawahi kuonyesha bastola yake hadharani kwa miaka yote aliyofanya naye kazi.

"Ni mwenye leseni ya kumiliki silaha, namfahamu kwa sababu nilikuwa naye wakati akienda kuomba leseni," Hamisi alisema.

Shahidi mwingine wa upande wa mashtaka Elvis Ogolla alisema alikuwa katika klabu hiyo kwenye sherehe kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na mbili usiku huo na kwamba hakuna kilichotokea.

"Ulikuwa usiku wa furaha. Nilikuwa na mpenzi wangu," Ogolla alisema.

Ilikuwa yapata saa kumi na mbili asubuhi mpenzi wake alipoondoka kwenye klabu. Ogolla hakuwa tayari kuondoka naye. Lakini alimfuata nje.

Aliporudi kwenye kilabu, alichukua zamu kuelekea msalani. Hapo ndipo mambo yalipoharibika.

"Niliona kila mtu akitoka nje ya klabu. Sikuwa nimetambua kilichotokea. Pia niliondoka," alisema.

Dereva Dereck Makhoha alisema alipigiwa simu na meneja wake, Bw Mwai, ambaye alimwambia akimbie katika eneo la kuegesha magari la klabu hiyo.

Alifanya kazi katika kilabu kama dereva wa gari. Ni Makhoha aliyemkimbiza DJ Evolve katika Hospitali ya The Nairobi asubuhi hiyo.

"Alipofika hospitalini, DJ Evolve alipokelewa na wauguzi. Babu Owino aliwafuata hospitalini," Makhoha alisema.

Muda mfupi baadaye, askari polisi walikuja na kuwaelekeza waende kituo cha polisi cha Kilimani.

Hakimu mkuu mwandamizi wa mahakama ya Nairobi Bernard Ochoi aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10 itakaposikizwa.